Ogiek waapa kuunga mkono uhifadhi wa msitu wa Mau
FRANCIS MUREITHI na JOHN NJOROGE
WAKAZI zaidi ya 5,000 wa jamii ya Ogiek wanaoishi mashariki mwa msitu wa Mau, wameapa kuunga mkono juhudi za serikali za kuwafurusha wakulima waliovamia msitu huo.
Katika mkutano uliofanyika eneo la Mariashoni kando na msitu huo katika kaunti ya Nakuru mnamo Jumamosi, jamii hiyo iliazimia kushirikiana na serikali kuhifadhi msitu huo kwa kutoa habari zitakazosaidia kuwatambua waliouvamia.
Hata hivyo mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii ya Ogiek, Bw Joseph Towet alisema jamii hiyo haipendezwi na jinsi serikali inawafurusha wale waliovamia msitu wa Mau kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
“Jamii ya Ogiek inaunga mkono kuhifadhiwa kwa msitu wa Mau lakini njia inayotumiwa kuwafurusha waliovamia msitu huo inakiuka sheria na haki za kibinadamu na inachangia kuongezeka kwa hali ya taharuki miongoni mwa wakazi wanaoishi kando na msitu huo,”akasema Bw Towett.
Aidha Bw Towet alitoa mwito kwa serikali kutafuta ardhi mbadala na kuwapa makazi waliotimuliwa katika msitu huu.
“Jamii ya Ogiek inayoishi katika eneo la Narok Kusini imeathiriwa pakubwa na vita vya kikabila baina ya jamii ya Wamaasai na Wakipsigis wanaozozana kuhusu umilikaji wa ardhi katika msitu wa Mau na nyumba zao zimechomwa na mali ya maelfu ya pesa kuangamia,” akasema Bw Towett.
Bw Towett alidai kuwa ikiwa serikali itaendelea kutumia nguvu kuwafurusha wale waliovamia msitu wa Mau hasa katika eneo la Narok Kusini basi huenda mpango huu ukaleta uhasama zaidi miongoni mwa jamii hizi mbili ambazo zimekuwa zikizozana kwa muda mrefu.
Wakati huo huo, Bw Towett alisema kuwa serikali haijatoa makataa rasmi ya kuwafurusha wote waliovamia msitu wa Mau katika eneo la Mashariki.
“Sisi kama jamii ya Ogiek tunaomba serikali itoe mikakati kabambe ya jinsi ya kuwafurusha wale wote walivamia msitu wa Mau na jinsi watakavyopewa makao mapya badala ya kutoa makataa kupitia kwa machifu kuwatisha wakazi wa Mariashoni na Nessuit,” akasema Bw Towett.
Alidai kuwa kwa zaidi ya miaka mitano serikali imepuuza jamii ya Ogiek kila mara wanapotafuta suluhisho la msitu wa Mau.
“Jamii ya Ogiek sasa inataka serikali kuwapa makao ya kudumu na kufutilia mbali stakabadhi zote za ardhi zilizitolewa kwa wanasiasa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini kwa njia isiyo halali” akasema Bw Towett.