Habari MsetoSiasa

Uhuru arejea nchini kimya kimya, ajifungia Ikulu kujadili ushuru

September 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

BAADA ya kurejea nchini kimyakimya mnamo Jumapili usiku, Rais Uhuru Kenyatta Jumanne alifanya kikao cha faraghani katika Ikulu ya Nairobi na kushauriana kwa siku nzima na uongozi wa bunge ukiongozwa na Spika Justin Muturi, maafisa wakuu wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Waziri Henry Rotich na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara kuhusu hatima ya mswada wa ushuru wa VAT kwa mafuta.

Japo Wakenya wengi walitarajia rais avunje kimya chake baada ya kurejea kutoka ziara yake ya siku kumi nje ya nchi, jana aliendelea kunyamaza na tulipokuwa tukienda mitamboni hakuwa ametamka lolote kuhusu ushuru huo ambao umepandisha gharama ya maisha.

Rais ana muda wa hadi kesho ktia saini mswada huo, au aurejeshe bungeni. Asipofanya hivyo, utakuwa sheria hali inayomaanisha kuwa utekelezaji ushuru huo wa ziada ya thamani (VAT) utaahirishwa hadi Septemba 1,2020 kulingana marekebisho yaliyopitishwa na wabunge

Ikulu ya Rais haijatoa taarifa yoyote kuhusu kurejea kwa Rais Kenyatta, ambaye kwa kawaida habari za kuwasili kwake anapotoka ng’ambo hutangazwa na kitengo cha habari za rais.

Hadi tulipokuwa tukichapisha gazeti jana, Ikulu ya Rais haikuwa imetoa taarifa zozote kuhusiana na mkutano na yanayoendelea kuhusu ushuru huo ambao umelaaniwa na wananchi.

Duru kutoka afisi ya Spika Muturi zilielezea uwepo wa mkutano huo.

Ongezeko la bei ya mafuta limeibua utata nchini huku wasafirisha mafuta wakifanya mgomo wiki jana na kisha mahakama kuu ya Bungoma ikatoa agizo la kusimamishwa kwa ushuru huo ambalo Serikali imepuuza.

Mnamo Alhamisi wiki jana, Waziri Rotich alifanya kikao na wakuu wa Bunge katika majengo ya bunge ambapo aliahidi kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo hivi karibuni baada ya kufanya msururu wa mikutano.

Wakenya wanasubiri kwa hamu kusikia msimamo wa Rais Kenyatta kuhusu ushuru huo na mzigo wa madeni.