• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
RASMI: Uhuru akataa kuondoa ushuru wa 16%, bei ya bidhaa kuzidi kupanda

RASMI: Uhuru akataa kuondoa ushuru wa 16%, bei ya bidhaa kuzidi kupanda

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi kwamba gharama ya maisha sasa itaendelea kupanda baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kutia saini Mswada wa Fedha Alhamisi ambao ulikuwa umesimamisha utekelezaji wa ushuru wa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta.

Rais ameurejesha mswada huo bungeni na taarifa akitaka ufanyiwe mabadiliko ili kurejesha kupengee kinachoruhusu utekelezaji wa ushuru huo wa ziada ya thamani (VAT).

Hatua ya Rais inajiri saa chache baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kuwasilisha mswada huo kwake ili aushughulikie.

Kwenye taarifa aliyotumwa kwa vyombo vya habari Alhamisi jioni na msemaji wa Ikulu Kanze Dena, mswada huo unaolenga kusimamisha utekelezaji wa ushuru wa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta, uliwasilishwa kwa Rais Alhamisi Septemba 13, 2018.

Hii ni siku 13 baada ya Bunge la Kitaifa kuupitisha mswada huo ambao unapendekeza kuwa ushuru huo wa zaida ya thamani (VAT) usimamishwa hao mwaka wa 2020.

“Spika wa Bunge la Kitaifa Septemba 13 aliwasilisha hati rasmi kuhusu Mswada wa Fedha nambari 20 wa 2018 ili ulishughulikiwe na Rais,” taarifa hiyo ya Bi Dena ikasema.

Wakenya wa matabaka mbalimbali wamekuwa wakimwekea Rais Kenyatta presha wakimtaka atie saini mswada huo ili kuzuia kupanda kwa bei ya mafuta, na kupanda kwa gharama ya maisha.

Serikali ilianza kutekeleza utozaji wa ushuru huo mnamo Septemba 1, kufuatia hatua ya Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) ya kutoa bei mpya zilizoakisi ushuru wa kima cha asilimia 16.

Wananchi wamekuwa wakiendelea kubebeshwa mzigo wa ushuru huo mpya licha ya mahakama kuu ya Bungoma kutoa amri ya kuusitisha ili kusubiri uamuzi wa Rais wa ama kuutia saini au kuurejesha bungeni.

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) imekuwa ikiishiniza serikali kuanza kutoza VAT kwa bidhaa za mafuta kama njia ya kuimarisha uwezo wake wa kulipa madeni ya kigeni ambao kwa sasa yamefikia Sh5.1 trilioni.

Lakini saa chache baadaye Rais alikataa kuutia saini, hatua ambayo imepelekea Spika Muturi kuitisha vikao viwili vya bunge la kitaifa Jumanne na Alhamisi wiki ujao kujadili sababu za Rais kuukataa mswada huo.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwa wabunge ambao watahitajika kubatilisha uamuzi wa Rais kwa kura 233, yaani thuluthi mbili ya wabunge wote 349.

You can share this post!

‘Baba’ apewa mlinzi rasmi wa serikali nchini...

Apigwa marufuku mechi 27 kwa kukwaruza kichuna wake kifuani

adminleo