Wahubiri wataka michango ya wanasiasa kanisani itolewe kisiri
Na VALENTINE OBARA
VIONGOZI wa dini nchini sasa wamependekeza kuwa michango ya wanasiasa makanisani na katika taasisi nyingine za kidini iwe ikitolewa kisiri.
Kupitia kwa muungano wao wa kujadili changamoto za kitaifa, viongozi wa dini mbalimbali walisema wanasiasa wakomeshwe kutangaza michango wanayotoa wakati wa harambee za taasisi za kidini ili taasisi hizo zisionekane kama kwamba zinafaidi kutokana na ufisadi au zinatakasa wafisadi.
Kwa muda mrefu, viongozi wa kidini hasa wa makanisa wamekuwa wakishambuliwa kwa maneno na baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa wanaochukizwa na mitindo hiyo ya wenzao, kwa kupokea mamilioni ya pesa ambazo hazijulikani zinakotoka.
“Taasisi za kidini hazifai kukubali michango hadharani kutoka kwa wanasiasa waliochaguliwa au viongozi wengine wa kisiasa wala maafisa wa kitaifa, ambayo hutolewa kwa shamrashamra kubwa. Michango kutoka kwa watu aina hii inafaa kutolewa kisiri na kibinafsi sawa na jinsi waumini wengine wote wanavyofanya,” wakasema, kwenye taarifa iliyochapishwa katika baadhi ya magazeti jana.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamewahi kujitokeza wazi kupinga jinsi makanisa yanavyopokea mamilioni ya pesa za wanasiasa ni Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter, na Kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance, Dkt Ekuru Aukot.
Mmoja wa wanasiasa mwenye umaarufu wa kutoa michango mikubwa ya pesa makanisani ni Naibu Rais William Ruto, ambaye amekuwa akipuuzilia mbali mahasimu wake wanaomhusisha na ufisadi.
Pesa za ufisadi
Hata hivyo, viongozi wa kidini wamekuwa wakijitetea kuwa ni vigumu kutofautisha kati ya pesa zilizopatikana kutoka kwa ufisadi, na pesa zinazopatikana kwa njia ya haki ambazo hutolewa wakati wa mchango.
Muungano huo wa kidini unajumuisha makundi mbalimbali kama vile Shirikisho la Kievanjelisti la Kenya, Baraza la Wahindu la Kenya, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kenya, Baraza la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu, Shirika la Makanisa ya Kiafrika, Kanisa la Kiadventista la Sabato, Chama cha Kiislamu cha Shia Ithnashari na Baraza Kuu la Waislamu la Kenya.
Mbali na suala hilo la ufisadi, muungano huo ulikariri misimamo yake kuhusu marekebisho ya katiba ambapo huwa unapigia debe kuundwa kwa nafasi zaidi katika kitengo kikuu cha utawala wa taifa ili kuwe na waziri mkuu na manaibu wake wawili.
Viongozi hao walipendekeza pia marekebisho ya katiba yafanywe ili mgombeaji urais anayeibuka wa pili katika Uchaguzi Mkuu awe akiachiwa wadhifa wa kiongozi wa upinzani katika bunge la taifa, na mgombea mwenza wake aongoze upinzani katika seneti, na tume maalumu ibuniwe kuongoza utekelezaji wa ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC).
Kuhusu ugatuzi, wamependekeza ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti uongezwe hadi kiwango kisichopungua asilimia 30.