Waboni walia maisha magumu huenda yakaangamiza jamii yao
NA KALUME KAZUNGU
WAZEE kutoka jamii ya Waboni, Kaunti ya Lamu, wanaitaka serikali ya kitaifa kufikiria kuangazia sekta nyingine muhimu za maendeleo zilizolemaa eneo hilo badala ya kujikita katika suala la usalama pekee.
Wazee hao kutoka vijiji vya Pandanguo, Jima, Bar’goni na Basuba wanasema sekta nyingi, ikiwemo ile ya elimu, ukulima, uchukuzi na miundomsingi zinazidi kusambaratika kila kuchao, hatua ambayo imepelekea umaskini kukithiri miongoni mwa Waboni.
Wakizungumza na Taifa Leo katika kijiji cha Pandanguo wakati wa kikao maalum cha kujadili hali na mwelekeo wa jamii hiyo Jumanne, wazee walieleza hofu kwamba huenda jamii yao imezwe na jamii nyingine na kuangamia kabisa siku za usoni iwapo serikali haitawapiga jeki katika masuala ya maendeleo endelevu.
Mwenyekiti wa Elimu katika jamii hiyo, Bw Ali Sharuti, alisema idadi kubwa ya wanafunzi kutoka jamii ya Waboni wamefukuzwa shule na wamelazimika kubakia nyumbani na wazazi wao kwa kukosa karo.
Alieleza haja ya serikali na wafadhili kuwadhamini Waboni, ikizingatiwa kwamba tangu operesheni ya usalama ilipoamriwa vijijini mwao, wakazi hawajaweza kujiendeleza kwa namna yoyote.
Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba, 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.
“Kuna zaidi ya wanafunzi 20 wa shule ya upili kutoka jamii yetu hapa Pandanguo pekee ambao wamekaa nyumbani kwa zaidi ya wiki mbili sasa baada ya kufukuzwa shuleni kwa sababu ya karo.Umaskini umekithiri. Hofu yetu ni kwamba huenda jamii yetu isambaratike kwa kukosa wa kuiendeleza siku za usoni. Kaunti na serikali kuu iangazie suala hili kwa uzito,” akasema Bw Sharuti.
Mmoja wa wazee hao, Bw Adan Golja, alisema tangu operesheni ya usalama ilipozinduliwa kwenye msitu wa Boni, wakazi hawajaweza kuruhusiwa kujitafutia kwenye msitu wao, jambo ambalo limezidisha ufukara na hali ngumu ya maisha kwa jumla.
Tangu jadi, Waboni hutambulika kwa maisha yao ya kutegemea msitu, ikiwemo kuchuma matunda ya mwituni, kuvuna asali na kuwinda wanyama pori.
“Serikali imeelekeza fikra na nguvu zake zote kwa suala la usalama ilhali sekta nyingi hapa zimefeli. Tunashukuru kwamba usalama umerejea. Watambue kuwa sisi tunahitaji kula, njaa imekithiri, watoto wetu wamekosa karo na pia barabara zetu ni mbaya. Haya ni mambo yanayofaa kuangaziwa pia,” akasema Bw Golja.
Naye Bw Hamisi Msuo aliiomba serikali kuhakikisha shule zao tano za msingi ambazo zilifungwa miaka minne iliyopita eneo la Basuba zinafunguliwa ili watoto wao waendeleze masomo kama wengine.
Shule za Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe zimesalia kufungwa tangu 2014 kufuatia visa vya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa magaidi wa Al-Shabaab.
Hali hiyo ilipelekea walimu waliokuwa wakihudumu kwenye shule hizo kutoroka kwa kuhofia usalama wao.
Waboni pia waliisisitizia serikali kuboresha barabara zao, ikiwemo ile ya Witu hadi Pandanguo na ile ya Hindi, Basuba hadi Kiunga ambazo ziko katika hali duni.