Wakenya watumia mafungu ya Biblia kukemea wabunge
Na PETER MBURU
GHADHABU ya Wakenya kufuatia hatua ya bunge kupitisha sheria ya kupandisha ushuru wa bidhaa muhimu imewapelekea kuamua kutumia vita vya imani dhidi ya wabunge waliounga mkono sheria hiyo.
Kufuatia hatua hiyo ambayo sasa itafanya baadhi ya bidhaa ambazo Mkenya wa kawaida hutumia kila siku kupanda bei kupindukia, Wakenya wameamua kuingia katika kitabu kitakatifu na kutoa baadhi ya mafungu ambayo yanaonya watunga sheria kutotesa wananchi.
Kupitia mitandao ya kijamii, Wakenya walionekana wakituma jumbe zilizotoa onyo kali kwa viongozi, zikitolewa moja kwa moja kutoka Biblia.
“Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; 2 ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! 3 Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? 4 Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa,” likasema fungu moja lililosambazwa zaidi kutoka kitabu cha Isaiah 10: 1-4.
“Kwa njia nyingine ya kueleweka hata zaidi, fungu hilo lilisema “Waangalie tu watunga sheria hao wanaotunga sheria mbovu na kufanya maisha magumu kwa watu. Hawatoi haki kwa masikini. Wanatwaa haki za masikini na kuruhusu watu kuibia wajane na mayatima. Watunga sheria lazima mtaelezea kile mmefanya. Mtafanya nini wakati huo? Kuangushwa kwenu kunakuja kutoka nchi ya mbali. Mtakimbilia wapi msaada wenu? Pesa zenu na utajiri hazitawasaidia. Mtainama kama wafungwa. Mtaanguka kama wafu, lakini hilo halitawasaidia. Mungu bado atakuwa na hasira na atawaadhibu,” fungu hilo likasema waziwazi.
Jumbe hizi zimekuwa zikisambazwa na Wakenya katika mitandao yote, wakieleza kuhusu namna walivyoghadhabishwa.