Ni dhambi kuu kutumia kondomu, Kanisa Katoliki laonya
Na WINNIE ATIENO
KANISA Katoliki limesema kamwe halitokubali waumini wake kukumbatia matumizi ya kondomu licha ya takwimu kuonyesha Kenya inaendelea kupata maambukizi mapya ya Ukimwi.
Maaskofu hao walipigia debe njia mbadala za kupunguza maambukizi ya maradhi ya ukimwi huku wakiwataka Wakenya kutojihusisha na tendo la ngono hadi wanapoolewa au kuoa kwa kuwa hiyo ni dhambi.
Wakihutubu Jumanne kwenye kongamano la kujadili maswala ya afya katika hoteli ya PrideInn Paradise jijini Mombasa, maaskofu hao wakiongozwa na askofu wa Dayosisi ya Kakamega Joseph Obanyi waliwataka Wakenya kushirikiana kuangamiza maaMbukizi ya ukimwi.
Swala tata la Ukimwi lilijadiliwa kwa kina huku wataalamu wa afya wakitaka hospitali kuhakikisha Wakenya wanapewa mafunzo bora ya Ukimwi yakiwemo kupimwa na wale wanaopatikana na maradhi hayo kupewa dawa za kupunguza makali ya HIV almaarufu ARVs.
Askofu Obanyi alisema Kanisa Katoliki litaendelea kupigana dhidi ya maambukizi ya gonjwa hilo.
“Kanisa lina mafunzo yake na wajua tumekuwa katika mstari wa mbele kukabiliana na jinamizi la ukimwi, hata hivyo utumizi wa kondomu si ajenda ya kanisa. Kanisa linataka kuhakikisha tunapunguza maambukizi ya ukimwi na tunawarai Wakenya kuepuka kutenda tendo la ndoa,” akasema Askofu huyo.
Aliongeza kuwa wanawafunza waumini kuepuka kujamiiana lakini matumizi ya kondomu si mojawapo ya mbinu faafu.
“Kanisa linaamini Wakenya wanaweza kujitokeza na kupimwa, lakini tunawafunza kutojiingiza kwenye maswala ya tendo la ndoa. Vilevile tunawapa watu wetu nasaha na tunawafunza umuhimu wa kujua hali zao,” akasema.
Kulingana na askofu huyo Kanisa Katoliki lina vituo 500 vya afya nchini na vituo vya kufunza maswala ya afya 22.
Walisema maambukizi ya Ukimwi yanaweza kudhibitiwa kwa njia nyingi.
“Kanisa linafunza mabaya na mazuri, na huwezi kuanza kufikiria jambo linaweza kufana sababu dunia inasema hivyo. Kwa hivyo pia sisi tulikumbatie. Nawapa changamoto, je, kondomu ndio njia pekee inayoweza kuzuia maambukizi ya Ukimwi? Je ni maadili mema?” akauliza.
Alisema mafunzo ya kondomu si maadili mema na kanisa haliwezi kufunza swala hilo.
Kulingana na Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Maambukizi ya Ukimwi, zaidi ya watu 28, 000 waliokuwa wakiishi na Ukimwi walifariki dunia kutokana na maradhi hayo mwaka 2017.
Baraza hilo pia lilisema kuwa zaidi ya watu milioni moja wanatumia dawa Za kupunguza makali ya ukimwi huku idadi ya watu wanaoishi na virusi hivyo ikisalia kuwa milioni 1.4.
Akiongea hivi majuzi kwenye kongamano muungano wa walimu wakuu wa shule za msingi nchini, mkurugenzi wa baraza hilo Dkt Nduku Kilonzo alisema takwimu hizo zinaonyesha Ukimwi bado ni changamoto nchini. Dkt Kilonzo alitaja unyanyapaa miongoni mwa changamoto kubwa zaidi.