Uhuru apiga marufuku samaki kutoka Uchina
Na PETER MBURU
RAIS Uhuru Kenyatta ameungana na Wakenya wanaolalamika kuhusiana na kuongezeka kupita kiasi kwa samaki kutoka China humu nchini, akisema hali hiyo imeumiza wafanyabiashara wadogo katika soko la samaki.
Akizungumza Jumanne wakati wa kikao na wafanyabiashara hao, Rais alisema kunafaa kuwekwa vizingiti kwa samaki kutoka China kuuzwa humu nchini, ili kuwaokoa wafanyabiashara wadogo kutokana na ushindani mkali ulioletwa na wale wanaotolewa China.
Rais Kenyatta alisema ni jukumu la serikali kuhakikisha inawakinga wafanyabiashara wadogo kutokana na kuuzwa kwa samaki hao humu nchini, kwa kuzuia kuingizwa kwao.
“Jameni, tunatoa samaki kutoka China, na wenzetu hapa wanaumia…,” akasema.
Rais Kenyatta alipendekeza hata serikali kutumia mbinu zozote ziwezekanazo kama kutoa madai kuwa samaki wa China hawajafikia viwango vifaavyo ili kuwazuia kuuzwa humu nchini.
“Hata kama Mswada wa Fedha umepita, lazima tufikirie kwa kina, tunaweza kusema hao samaki wamefika ni wabaya na tunawafungia (kuuzwa humu nchini). Kuna njia nyingi serikali inaweza kufanya kazi ndiyo tuhakikishe kuwa watu wetu wamefaidika if kiwa kwa kweli tunaazimia kuwahudumia,” akasema Rais Kenyatta.
Maneno yake yalikuja wakati vilio kutoka kwa wafanyabiashara wadogo vimekuwa vikizidi kuhusu kuongezeka kwa samaki kutoka China katika soko la taifa.
Baadhi ya samaki hao wamekuwa wakidaiwa kuwa wa plastiki, jambo ambalo limekuwa likizua hofu miongoni mwa Wakenya watimizi wa mlo wa samaki.