Habari Mseto

Uhuru atoa sababu za kupiga marufuku samaki wa Uchina

October 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepiga marufuku uagizaji wa wa samaki kutoka China. Kiongozi wa taifa alisema samaki kutoka China wanaharibu soko la samaki wanaovuliwa na wavuvi wa humu nchini.

Alisema hayo  Jumanne alipofungua rasmi kongamano kuhusu wafanyabiashara wadogo wadogo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Strathmore, Nairobi.

“Nimeelezwa kuhusu samaki ambao huingizwa nchini kutoka China. Hatufai kuagiza samaki wa kutoka China ilhali wavuvi wetu huvua samaki kwa wingi humu nchini,” akasema.

Rais Kenyatta alisema japo Mswada wa Fedha wa 2018 ulipendekeza nyongeza ushuru kwa bidhaa mbalimbali kutoka humu nchini, hiyo haimaanishi kuwa tunafaa kuagiza bidhaa ambazo zinapatikana katika masoko yetu.

Kauli yake inajiri wakati ambapo kumekuwa na kilio kutoka kwa wavuvi wa humu nchini na wafanyabiashara wa samaki kuhusu uwepo wa samaki kutoka China katika masoko ya humu nchini.

Ilidaiwa kuwa samaki hao huagizwa na wafanyabiashara kwa misingi kuwa huwa ni wa bei rahisi ikilinganishwa nma samaki wanaovuliwa humu nchini.

Mnamo Juni mwaka huu wavuvi wanaohudumu katika ziwa Naivasha walilalamikia wingi wa samaki kutoka China katika masoko ya humu nchini hali ambayo ilikosesha samaki wao wateja. Waliitaka serikali kuu kuingilia kati suala hilo.

Na mwaka 2017, aliyekuwa Gavana wa Kisumu Jack Ranguma aliitaka Serikali kupiga marufuku samaki kutoka China.

Hata hivyo, Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) ilisema samaki huagizwa kutoka China kwa sababu uzalishaji wa samaki humu nchini hautoshelezi hitaji la soko ambayo inapanuka kila uchao.