Habari MsetoSiasa

Wafanyabiashara kutoka Uchina wazimwe kabisa – Wabunge

October 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge kutoka Mlima Kenya wamezitaka serikali za kaunti zisitoe leseni za kibiashara rejareja kwa wageni wakisema biashara hizo zinapaswa kuachiwa Wakenya.

Wabunge saba hao haswa walikerwa na mwendo wa Wachina kuingilia biashara za rejareja ambazo walisema zinafaa kuendeshwa na Wakenya, haswa vijana ambao wengi wao hawana ajira licha ya kuhitimu kwa shahada mbalimbali masomoni.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wabunge hao saba pia waliitaka Serikali ya Kitaifa kufutilia mbali vyeti vya kazi kwa wageni ambao hufanyakazi ambazo Wakenya wamehitimu kufanya.

“Asilimia 55 ya vijana nchini hawana ajira. Hii ndio wengi wao wameingilia biashara ndogo ndogo za uchuuzi. Hatatuka watu kutoka China kuja hapa nchini na kushindana na watu wetu katika biashara ya kuuza bidhaa ambazo zimetengenezwa kwao na kuingizwa humu nchini,” akasema jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Kwa hivyo, tunazitaka serikali zote za kaunti, zikiongozwa na Serikali ya kaunti ya Nairobi kufutilia mbali leseni za kibishara kwa Wachina hao ambao wamezagaa katika miji kadhaa nchini wakishindana na Wakenya,” Bw Nyoro akaongeza.

Naye Mbunge wa Kiambu Mjini Bw Jude Njomo alimtaka mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu Biashara Bw Kanini Kega kufuatilia suala hilo na maafisa husika katika serikali kuu na zile za kaunti ili kuhakikisha kuwa masihali ya wafanyabishara wa asilii ya Kenya yanalindwa.

“Ikiwa hakuna Mkenya ambaye huruhusiwa kufanya biashara nchini China, mbona Wachina wapewe nafasi hiyo humu nchini huku watu wetu wakiseka. Tunataka Bw Kega na kamati yake kuhakikisha kuwa biashara zote za reja reja zinaendesha na Wakenya wala sio wageni,” akasema.

Mbw Nyoro na Njomo walikuwa wameandamana na wabunge wenzao, James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Catherine Waruguru (Mbunge Mwakilishi wa Laikipia), Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu), Benjamin Mwangi (Embakasi ya Kati) na Joseph Kiai (Mukweini).