NEMA yanasa mifuko ya plastiki kutoka Tanzania
Na Winnie Atieno
HALMASHAURI ya mazingira ya kitaifa (Nema), imenasa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku iliyoagizwa kutoka nchi jirani ya Tanzania. Mifuko hiyo ipatayo 8.5 milioni ilinaswa ilipokuwa ikipakuliwa katika kampuni moja ya basi katikati mwa jiji la Mombasa.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Nema katika kaunti ya Mombasa Stephen Wambua, mwagizaji wa bidhaa hizo zilizopigwa marufuku humu nchini ametoweka.
“Lakini anasakwa na polisi, aliagiza tani 1.7 ya mifuko ya plastiki ilhali Kenya ilipiga marufuku mifuko hiyo,” Bw Wmbua alisema.
Bidhaa hiyo ilinaswa kwenye operesheni kali baina ya polisi na maafisa wa Nema katika kituo hicho cha basi.
“Ndipo tukapata mifuko hiyo ilipakuliwa kutoka kwenye basi la Simba coach KBU 343C katika afisi zao za Mwembe Tayari,” akasema Bw Wambua.
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu Bw Wambua alisema mwenye bidhaa hiyo ambaye anasakwa anajulikana kwa jina Bw Issa alihepa kwenye uvamizi huo.
“Bidhaa hizo zilipelekwa katika kituo cha polisi cha Central huku juhudi za kumsaka kwenye mizigo hiyo zikiendelezwa na polisi,” alisema Bw Wambua.
Aidha alionya wenye mabasi kuwa makini wasitumike kuingiza bidhaa zilizopigwa marufuku humu nchini.
Pia alionya wakazi Mombasa dhidi ya kutumia mifuko ya plastiki.
“Badala yake munaweza kutumia mifuko ambayo haiharibu mazingira yetu,” akaongeza.
Haya yanajiri huku wafanyibiashara katika soko wakiendelea kutumia mifuko kufungia wakazi bidhaa walizonunua hususan katika soko la Kongowea.