Ndege ya kwanza ya Kenya yatua Marekani baada ya saa 15 angani
Na WANDERI KAMAU
NDEGE ya Kenya iliyofanya safari ya kwanza ya moja kwa moja kati ya Kenya na Marekani, jana ilitua salama salimini katika uwanja wa kimataifa wa ndege John F Kennedy jijini New York.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 ya shirika la Kenya Airways ilitua mwendo wa saa nan e mchana saa za Afrika Mashariki, baada ya safari za saa 15. Ilikuwa imeondoka uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi usiku wa Jumapili, mwendo wa saa 5.20 usiku.
Safari hiyo ni ya kihistoria, kwani ni mara ya kwanza ambapo abiria wanasafiri moja kwa moja hadi Amerika kutoka Kenya.
Ufanisi huo unafungua ukurasa mpya katika safari za ndege nchini, ikizingatiwa kuwa hakujawahi kuwa na ndege inayosafiri moja kwa moja hadi Marekani bila ya kupitia miji mingine ulimwenguni.
Na ijapokuwa ndege hiyo ilikuwa imepangiwa kuondoka saa 4.45 usiku mnamo Jumapili, ilichelewa dakika chake.
Kwa kawaida, safari ya kawaida ya ndege kati ya Kenya na Amerika huchukua saa 22. Lakini katika hali ya sasa, abiria watakuwa wakichukua saa 15, ikiwa na maana kuwa muda huo unapunguzwa kwa saa saba.
Akizungumza muda mfupi kabla ya ndege hiyo kuondoka, Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa safari hizo zinaiwzesha Kenya kupanuka kibiashara na sekta ya utalii.
“Hii ni siku ya kihistoria kwa sekta ya uchukuzi wa ndege nchini. Safari hizo za moja kwa moja zitaimarisha sana sekta muhimu kama utalii na kuimarisha mahusiano yetu na wengine duniani,” akasema Bw Kenyatta.
Kenya Airways ndiyo kampuni ya kwanza kuwa na safari za moja kwa moja kwenda Marekani katika ukanda wa Afrika Mashariki. Baadhu ya sehemu ambazo huwa inasafiri ni Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati, India na bara Asia. Kampuni hiyo ilitoa video iliyoonyesha ndege hiyo ikiwasili na kukaribishwa kwa shangwe.