• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Sh2 bilioni za upanzi wa miti zatoweka

Sh2 bilioni za upanzi wa miti zatoweka

Na WANJOHI GITHAE

WIZARA ya Mazingira inamulikwa kuhusiana na namna ilivyotumia Sh2 bilioni za kutumika katika upanzi wa miti shuleni, katika mradi alioanzisha Rais Uhuru Kenyatta miaka mitano iliyopita.

Barua ambazo Taifa Leo imeziona zinaonyesha kuwa Shirika la Kusimamia Misitu nchini (KFS) ambalo lilijukumiwa kuendesha shughuli hiyo limeondolewa katika mradi wenyewe na wizara.

Mradi huo ulinuia kupanda miti katika shule za msingi za umma kama mbinu ya kuongeza idadi ya miti nchini, lakini sasa KFS imeandikia wizara barua nyingi ikitaka kujua namna pesa zilizotolewa na serikali zinatumika hazijajibiwa.

Lakini imebainika kuwa kampuni moja inayomilikiwa na mtu wa familia ya Rais Uhuru Kenyatta ilipewa zabuni ya kusambaza miche ya Sh3 milioni ila ilikataa biashara hiyo.

Kampuni ya James Hauling Ltd, ambayo wakurugenzi wake ni James Muigai Ngengi na Marthe Muigai iliandikia katibu katika wizara ya Mazingira Margaret Mwakiama mnamo Machi 2017 ikikataa biashara hiyo.

“Tunataka kubainisha kuwa hakuna aliyeomba zabuni hii ama akaomba kusambaza miche kwa njia yoyote kwa wizara yenu ama idara nyingine yoyote ya serikali iwe ni sisi ama mwanachama yeyote wa Jam Hauling Company Ltd,” wakurugenzi waliandika.

Mradi huo uliidhinishwa na Rais Kenyatta Desemba 2013, lengo lake likiwa kupanda miti katika shule 5,000 za umma kufikia mwisho wa miaka mitano.

Lakini kulingana na barua aliyoandika mwenyekiti wa bodi ya KFS Joseph Kinyua, mradi huo unaonekana kama uliosambaratika na kufeli.

“Japo nakala za mradi zilitambua KFS kuwa mtekelezaji mkuu wa mradi nayo wizara kukagua na kuongoza kamati ya kuuendesha, pesa za kutekeleza mradi hazijawahi kufika kwa KFS,” Bw Kinyua akamwandikia katibu wa sasa katika wizara ya Mazingira Susan Mochache mnamo Septemba 17, 2018.

Kwenye barua hiyo, mwenyekiti huyo anaendelea kumkumbusha kuwa amekuwa akiandikia wizara hiyo bila kupokea jawabu.

Lakini Bi Mwakiama jana alisema kuwa alipokuwa ofisini kati ya 2016/17, wizara ilipokea Sh500milioni ambazo ilitumia kupanda miti katika shule 205, idadi nusu ya shule ambazo bunge lilikuwa limetengea pesa hizo.

Kupitia barua Januari mwaka uliopita, aliyekuwa waziri Profesa Judy Wakhungu alikiri kuwa pesa hizo zilifaa kutumwa kwa KFS itekeleze mradi huo.

You can share this post!

Mzee Moi amuita Kalonzo kwa mazungumzo

Korti yazima mawakili waliopinga NMG ikiripoti kesi ya NYS

adminleo