Habari Mseto

AFYA: Wenye mapato ya chini wazidi kufaidika na matibabu ya bure

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

GHARAMA ya maisha inayopanda kila uchao humu nchini sasa imewasukuma wakazi wa mabanda ya mijini kukoma kulipia ada za Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) na kuweka afya yao hatarini.

Familia nyingi sasa zimepangia ada hiyo ya Sh500 kwa mwezi sasa kwa matumizi mengine ya kinyumbani, hali inayowaacha bila kinga ya bima ya NHIF iwapo mtu ataugua ghafla ugonjwa unaohitaji fedha nyingi kutibiwa.

Ni kutokana na hali hii ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali yamepenyeza katika mitaa ya mabanda na kuwapa wakazi huduma ainati za matibabu bila malipo.

Miongoni mwa mashirika hayo ni Jubilant Stewards of Africa (JSA) na International Health Operations Patients Education and Empowerment (IHOPEE) kutoka Amerika ambayo yameingia kwa mkataba kutoa huduma za bure za matibabu kwa maelfu ya wakazi wenye mapato ya chini jijini Nairobi na Kisumu.

Wakihutubia wanahabri katika afisi zao eneo la Mombasa Road, Nairobi, maafisa kutoka mashirika yote waliahidi kuzidisha hisani yao kwa watu maskini, huku wakiwa tayari wametoa huduma hizo kwa wakazi zaidi ya 1,200 mitaani Imara Daima, Nairobi na Agoro, Kisumu.

Kulingana na ushuhuda wa wagonjwa, mpango huo umewaleta karibu na huduma za afya ambazo kwa muda mrefu zimekuwa ghali kwao.

Mkazi wa eneo la Rarieda, Dickens Wara ambaye amekuwa akiugua malaria alionyesha furaha yake baada ya kupokea dawa mjini Kisumu.

“Nimekuwa mwele kwa muda lakini sikuweza kupata hela za matibabu. Vituo hivi vya huduma za afya vimekuja kwa wakati ufaao. Tangu nianze kutumia dawa nilizopewa, nahisi mwili wangu umepata nguvu na kunipa afueni,” akasema.

Maisha ya John Odoro yametekwa na maradhi ya niumonya au kichomi lakini tangu awatembelee madaktari kwenye vituo hivyo jijini Kisumu, kwa sasa anakaribia kupona.

Wakazi walijitokeza kwa wingi kupata matibabu bila malipo mtaani Imara Daima, Nairobi. Picha/ Faustine Ngila

“Ninawaomba waandalizi wa huduma hizi kufanya hivyo kote nchini kwa Wakenya wengi ambao hawawezi kumudu bei ya NHIF wala malipo ya hospitalini,” akasema Bw Odoro.

Mwakilishi wa Kenya wa shirika la Ihopee Askofu Silas Kanali alisema huduma hizo zitafanyika katika mtaa wa Kayole hapo Jumatano na Alhamisi mwezi huu kabla ya kuwafaa wakazi wa Mukuru Kwa Njenga ndipo warudishe wema huo katika mabanda ya Kisumu.

“Lengo letu ni kuwafikia watu wote ambao hawawezi kupata pesa za kulipia huduma ghali za matibabu,” akasema.

Huduma zinazotolewa kwenye vituo ni pamoja na vipimo vya saratani, chanjo za watoto, vipimo vya Ukimwi. Magonjwa kama malaria, niumonia, kisukari, ugonjwa wa mifupa na shinikizo la damu yanatibiwa.

“Tungependa kuona jamii ambayo watu wote, maskini kwa matajiri wanaweza kupata huduma za kiafya kwa usawa. Vituo vyetu vi wazi kwa yeyote ambaye ameshindwa kufika hospitalini akiogopa gharama ya juu,” akasema mkuu wa mawasiliano wa shirika la Jubilant Stewards of Africa, Bw Jared Oluoch Oundo.

Ushirikiano huu unatarajiwa hatimaye kufikia Wakenya katika pembe zote za nchi na kutokomeza maradhi kwenye vitongoji na kuweza kupunguza kiwango cha maambukizi.

“Tuna madaktari 15 kutoka mataifa ya Amerika, Canada na Misri ambao watawahudumia wagonjwa 600 kwa siku.”

Ihopee ni shirika lililoanzishwa na Wakenya watatu wanaoishi Amerika ambao wamejitolea kuzifaa kiafya familia maskini kote nchini, kama ishara ya zawadi kwa jamii.

“Jubilant Stewards of Africa ni shirika ambalo kaulimbiu yake inalenga kuwaelimisha vijana kuhusu nafasi za kazi, hali zao za kiafya na ujasiamali,” akasema mkuu wa kitengo cha teknolojia Bw Mark Alex.