• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Mtapokea mamilioni yenu Machi 2019, Harambee Stars yaambiwa

Mtapokea mamilioni yenu Machi 2019, Harambee Stars yaambiwa

Na GEOFFREY ANENE

AHADI ya Harambee Stars kuzawadiwa na serikali Sh50 milioni ikifuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019 ambayo ilitolewa na Naibu Rais William Ruto mwezi Oktoba 2018 itatimizwa Machi mwaka 2019.

Aidha, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liko na bajeti ya Sh200 milioni ya kushughulikia Harambee Stars kabla ya AFCON, wakati wa mashindano haya na pia kuizawadia kutegemea umbali itafika kwenye mashindano hayo ya mataifa 24.

Tangu Stars ichukue usukani wa Kundi F baada ya kukaba Ethiopia 0-0 mjini Awasa mnamo Oktoba 10, mashabiki wa Kenya wamekuwa wakitaka serikali iipe timu hiyo haki yake. Miito ya kutaka Stars ipokee zawadi hiyo iliongezeka pale ilipochapa Ethiopia 3-0 katika mechi ya marudiano jijini Nairobi mnamo Oktoba 14.

Wengi wa Wakenya waliamini Stars imeshafuzu kushiriki AFCON 2019 kwa sababu Sierra Leone ilikuwa imepigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) mnamo Oktoba 5.

Hata hivyo, CAF ilijikokota kutangaza hali ya kundi F hadi Novemba 30. Baada ya CAF kutoa hakikisho Kenya pamoja na nambari mbili kwenye kundi hilo, Ghana, zimefuzu, FKF sasa imesema itakuwa vigumu kugawana fedha hizo hadi wachezaji watakapokusanyika jijini Nairobi wakati wa kipindi cha mexhi za kimataifa mwezi Machi mwaka 2020.

Kulingana na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa mikakati jinsi fedha hizo kutoka kwa Serikali zitagawanywa bado inafanywa.

“Wizara ya Michezo imekuwa ikisubiri thibitisho kwamba Kenya imefuzu ndiposa ishughulike zawadi hiyo ya Sh50 milioni kwa Stars. Naona ile ahadi ya Sh50 milioni kwa Stars itatimia mwezi Machi mwaka 2019 baada ya mechi ambayo tunapanga ya kutoa shukrani kwa mashabiki wetu jijini Nairobi. Mechi hii itakuwa baada ya ile mechi ya mwisho ya Harambee Stars ya kufuzu kushiriki AFCON dhidi ya Ghana. Kabla ya wakati huo, itakuwa vigumu kwa sababu wahusika wengi wakuu ambao ni wachezaji hawako nchini,” Mwendwa amesema jijini Nairobi.

Mechi ya kushukuru mashabiki inatarajiwa kusakatwa Jumanne ya kwanza baada ya Kenya kuvaana na Ghana ambayo ni Machi 26. Kenya itazuru Ghana mnamo Machi 22 kwa mechi ya mwisho ya kundi F ambayo itaamua mshindi wa kundi hili. Kenya na Ghana zinashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama saba na sita, mtawalia. Ethiopia ina alama moja baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Sierra Leone hapo Septemba 9 kufutiliwa mbali.

Aidha, Mwendwa amesema FKF inashughulikia jinsi fedha FKF itagawana na Stars marupurupu. Amesema tayari kuna mpango jinsi benchi la kiufundi litapokea marupurupu. Kiasi cha bonasi kitategemea umbali Stars itafika.

“Kila hatua ambayo Stars itapiga katika AFCON, bonasi ya benchi la kiufundi itaongezeka kwa kiwango fulani ambacho tumeshakubaliana nalo. Tunataka pia mpango huo utumike pia kwa wachezaji,” amesema Mwendwa kabla ya kuongeza kwamba FKF pia itakuwa ikipokea kitu. “Tumekuwa tukiangalia jinsi mataifa mengine yanashughulikia suala hili la kugawana fedha na timu ya taifa.

Nchi kama Argentina kwa mafano, ina sheria ya asilimia 60-40. Asilimia 60 ya tuzo inaenda kwa timu nayo asilimia 40 inatumiwa na shirikisho kuendesha mipango yake. Sisi tunajadiliana kuhusu aslimia 70-30, ingawa kocha atakuwa na usemi jinsi tuzo ya wachezaji inavyogawanywa kwa sababu kuna wachezaji ambao wamesakata mechi zote za kufuzu, wengine moja ama mbili, wengine wamesakata mechi chache lakini mchango wao umekuwa mkubwa sana katika kampeni yetu ya kufika AFCON, na kadhalika.

Wakati wa Kombe la Afrika ya Kati na Mashariki (Cecafa) mwezi Desemba mwaka 2017, mpango uliokuwepo ni ule wa asilimia 80 ya tuzo kuendea timu na asilimia 20 kwa shirikisho.

Kenya, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya Cecafa, iliibuka mshindi na kuzawadiwa Sh10 milioni. Kwa kufuzu kushiriki AFCON 2019, Kenya tayari imejihakikishia tuzo ya Sh48,751,625 kutoka kwa CAF ikiwa itavuta mkia katika mechi za makundi.

You can share this post!

Kenya yakataa kuandaa AFCON 2019 kutokana na viwanja duni

Asante Kotoko ya Ghana yajiandaa kulimana na Kariobangi...

adminleo