Watalii wajumuika na wakazi kwa matibabu ya bure
NA KALUME KAZUNGU
HAFLA ya mwaka huu ya Maulid ya Lamu iliyokamilika mwishoni mwa juma iliwanufaisha pakubwa watalii na wenyeji zaidi ya 1500, ikiwemo watoto na watu wazima ambao walipokea matibabu ya bure kutoka kwa madaktari kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Matibabu hayo yaliandaliwa chini ya mwavuli wa Kamati Andalizi ya hafla ya Maulid ya Lamu ambayo ni ya awamu ya 131 tangu kuzinduliwa kwake.
Wakazi walipimwa maradhi tofauti tofauti na pia kupokea ushauri wa kimatibabu uliokuwa ukitolewa na madaktari spesheli, ikiwemo wale wa kutoka nchini Uturuki.
Miongoni mwa maradhi yaliyokuwa yakipimwa na ushauri nasaha kutolewa kwa wagonjwa ni pamoja na kifua kikuu, shinikizo la damu, kisukari, Ukimwi, matatizo ya meno na macho.
Waliopatikana na magonjwa walitibiwa ilhali wale ambao hawangeweza kutibiwa papo hapo waliandikiwa rufaa kwenye hospitali za nje ya Lamu.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo punde baada ya Maulid kukamilika, Afisa Msimamizi wa shughuli hiyo, Bw Ahmed Badawi, alisema Maulid ya mwaka huu ilifana pakubwa kwani wakazi ambao hawangeweza kugharimikia tiba kwa magonjwa mbalimbali waliweza kupokea matibabu ya bure bilashi kutoka kwa madaktari na wataalamu wa matibabu kutoka mataifa ya ng’ambo.
Alisema Maulid ya mwaka huu ilikuwa na sura mbili kwani mbali na waumini kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Mohamed (S.A.W) kuna wale ambao hata si waumini wa dini ya kiislamu ambao pia walinufaika kwa kupokea tiba wakati wa Maulid.
Kulingana na Bw Badawi, zaidi ya wataalamu 40 wa matibabu kutoka mataifa ya nje walifika Lamu ili kutoa huduma zao kwa waliohitaji bila malipo yoyote.
“Tunashukuru kwamba wageni, wenyeji na watalii walipokezwa matibabu ya bure na wataalamu wa matibabu zaidi ya 40 waliokuwa wamehudhuria hafla ya Maulid mwaka huu. Naweza sema kwa makadirio zaidi ya wenyeji, wageni na watalii 1,500 walifaidika na kambi za matibabu zilizokuwa zikiendelea wakati wa Maulid,” akasema Bw Badawi.
Naibu wa kamati andalizi ya sherehe hizo, Sharif Hussein alisema azma yao ni kuhakikisha sherehe hizo zinafana zaidi miaka ijayo kwa kupanua zaidi maeneo ambayo tiba za wagonjwa zitakuwa zikitekelezwa wakati wa Maulid.
“Najua kuna wagonjwa kutoka maeneo ya visiwani, ikiwemo Faza, Pate, Tchundwa, Kiunga, Ndau, Kizingitini na maeneo mengine ambao hawangeweza kufika mjini Lamu kupokea matibabu yaliyokuwa yameandaliwa wakati huu wa maadhimisho ya Maulid. Azma yetu ni kuhakikisha wakazi hao wanafikiwa kwani tutapeleka kambi za matibabu mahali waliko wakati Maulid ikiendelea hapa kisiwani Lamu miaka ijayo,” akasema Bw Hussein.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo walisifu mpango huo wa matibabu ya bure ambao huandaliwa kila mwaka wakati wa maadhimisho ya hafla ya Maulid.
Bi Halima Omar aliutaja mpango huo kuleta afueni hasa kwa wakazi wasiojiweza.
“Matibabu ya bure ni mpango mzuri na tumeufurahia sana. Kuna wengi ambao ni wagonjwa lakini kwa sababu ya umaskini, hawajaweza kupima wala kutibiwa maradhi wanayougua. Kambi za matibabu zilizoandaliwa wakati wa Maulid zimewezesha watu kutoka jamii maskini pia kupata matibabu kwani hakuna malipo yoyote yanayoitishwa,” akasema Bi Omar.
Hafla ya mwaka huu ya Maulid ya Lamu ilishuhudia idadi kubwa ya waumini wa dini ya kiilsamu, wageni na watalii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kimataifa waliohudhuria hafla hiyo ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Maulid huandaliwa kila mwaka na baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu ili kukumbuka kuzaliwa kwa Nabii Mtume Mohamed (S.A.W) katika mji mtakatifu wa Mecca katika mwaka wa 570AD.