Habari Mseto

Walimu wataka Sh17b za bima ya matibabu

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na OUMA WANZA

WALIMU wanataka watengewe pesa zaidi za bima ya afya wakisema Sh5.6 bilioni wanazotengewa kwa wakati huu hazitoshi.

Kupitia chama chao cha The Kenya National Union of Teachers (Knut) walimu hao wanataka Wizara ya Fedha kutengea walimu wapatao 312,060 kote nchini Sh17 bilioni kwa mpango huo.

“Hatuelewi kwa nini walimu zaidi ya 300,000 walioajiriwa na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) wanaweza kutengewa Sh5.6 bilioni za matibabu ilhali maafisa wa polisi 80,000 wanatengewa Sh5.3 bilioni kwa mpango huo,” inasema ripoti ya Knut inayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa 61 wa wajumbe jijini Nairobi Jumatano ijayo.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion inasema kwamba upatikanaji wa huduma bora za matibabu hutegemea kiwango ch pesa zilizotengwa. Knut ilikuwa ikitarajia Sh17 bilioni kila mwaka ili kuwezesha TSC kujadili na kampuni za bima ya afya ili walimu wapate huduma bora.

Chama hicho sasa kinataka Wizara ya Fedha kuchunguza upya pesa za bima ya afya na kuziongeza ili kuwezesha walimu kupata huduma bora za matibabu.

“Pia, tunataka TSC iendelee kusukuma Wizara ya Fedha itenge pesa zaidi za mpango wa matibabu. Zaidi ya yote, tume inafaa kuanzisha kitengo cha kusimamia mpango wa matibabu ya walimu,” inasema ripoti hiyo.

Aidha, Knut kinataka Wizara ya Fedha iwe ikitoa pesa kwa TSC ili iweze kuziwasilisha kwa kampuni za bima kuepuka fedheha ya walimu kukosa kuhudumiwa na hospitali kwa sababu ya pesa kutolipwa. Kulingana na TSC, walimu wote nchini wana bima ya matibabu kupitia kampuni ya Minet ambayo imekuwa ikitoa huduma hizo kwao kwa mwaka wa nne sasa.

Tume inasema kuna walimu 276,707 ambao wanategemewa na watu huku 173,892 wakiwa wachumba wao na watoto 500, 998. Kwa jumla, TSC inasema kuna watu 983,363 wanaofaidika moja kwa moja na mpango huo wa bima ya matibabu.

Asilimia 90 ya walimu wana watu wanaotegemea mpango huo huku asilimia 50 ya wanaonufaika na mpango huo wakiwa wanawake. Kila familia ya mwalimu kuna watu watatu wanaonufaika na mpango huo. Ripoti hiyo inasema kwamba tangu mpango huo uanze kutumika, kuna watu 136,964 waliolazwa hospitalini. Watu 158 hulazwa kila siku na 4376 hutibiwa na kurudi nyumbani,” inasema ripoti hiyo.

Inaeleza kuwa mpango huo umeokoa maisha kwa kusaidia waathiriwa wa ajali kwa kutumia ambulensi na hata kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Watu 139 wamepelekwa ng’ambo kwa matibabu 71 wakiwa walimu na 68 wakiwa watu wanaotegemea walimu.