Michezo

Mwanzo wa mwisho wa Messi na Ronaldo

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

NA CHRIS ADUNGO 

MWANZONI mwa Desemba, kiungo Luka Modric wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia alitawazwa mshindi wa taji la Ballon d’Or ambalo hutolewa kila mwaka kwa mwanasoka bora zaidi duniani.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 2007 kwa taji hilo kumwendea mchezaji tofauti baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kuyatawala makala yote ya hivi karibuni kwa kubadilishana ubingwa wa taji hilo kwa kipindi cha miaka 10.

Mnamo Septemba 2018, Modric alitawazwa Mchezaji Bora wakati wa kutolewa kwa tuzo za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na kutoa ishara za kutia kapuni ufalme wa Ballon d’Or.

Mbali na Modric, wachezaji wengine ambao walipigiwa upatu kutia kibindoni taji la Ballon d’Or mwaka huu, ni mshambuliaji shupavu wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane pamoja na chipukizi Kylian Mbappe aliyeambulia nafasi ya tatu mbele ya Ronaldo na Messi.

Kwa namna ambavyo taji la Ballon d’Or limekuwa likitolewa kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, wasimamizi wa tuzo hiyo walitufanya kusadiki kuwa ni Messi na Ronaldo pekee ndio wachezaji bora zaidi duniani. Ingawa sina kusudi la kupinga maamuzi hayo ambayo kwa mtazamo wangu ni ya kweli, basi ni nani mchezaji wa tatu bora zaidi duniani anayestahiki kuorodheshwa nyuma ya Messi na Ronaldo?

Japo nachochewa kumtaja mvamizi wa zamani wa Barcelona, Neymar Jr, huu ni uamuzi mgumu kwa kuwa wapo wachezaji wengine wazuri sana ambao viwango vyao vya ubora vinakaribiana mno.

Isitoshe, nafasi ya tatu katika tuzo za Ballon d’Or imekuwa ikitwaliwa na wachezaji tofauti tofauti kila mwaka tangu 2007 ambapo fowadi wa Brazil, Kaka alitawazwa mshindi akivalia jezi za AC Milan.

Sawa na Luis Suarez aliyetisha hapo awali kambini mwa Liverpool na Barcelona, Kevin De Bruyne na Mohamed Salah walikuwa nguzo na injini madhubuti kambini mwa waajiri wao muhula uliopita.

Salah aliwatambisha Liverpool na kuvunja rekodi nyingi za ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu jana. Naye De Bruyne aliyeshirikiana vilivyo na Sergio Aguero, alionesha mchezo wa kuridhisha mno ndani ya jezi za Man-City waliotawazwa mabingwa.

Hata hivyo, muda wa mwaka mmoja au hata miwili ni mfupi sana kumwezesha mtu kupima ushawishi, kukadiria ubora na kutathmini uwezo wa mchezaji.

Nahodha na kiungo wa Chelsea na timu ya taifa ya Ubelgiji, Eden Hazard amekuwa katika kiwango kizuri ugani kwa misimu michache iliyopita. Nyota huyo ambaye kwa sasa anahusishwa pakubwa na Real Madrid hata yuko hata juu ya Neymar, ila mvamizi huyu mzawa wa Brazil amekuwa mzuri mno katika misimu kadhaa iliyopita kambini mwa Barcelona.

Neymar ambaye hakujivunia kampeni za kuridhisha katika fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka huu, aliambulia nafasi ya tatu katika tuzo za Ballon d’Or mnamo 2015 na 2017 mtawalia.

Japo naamini kiwango cha Neymar kina uwezo wa kuboreka ndani ya PSG, tamanio la mwanasoka huyo kwa sasa ni kurejea Barcelona kwa imani kwamba atajitoa katika kivuli cha Messi na utawazwa Mchezaji Bora duniani.

Japo Mbappe anatarajiwa kuwarithi Messi, Ronaldo na Modric katika jitihada za kunyanyua taji la Ballon d’Or katika miaka kadhaa ijayo, Mfaransa huyo atajipata katika ushindani mkali hasa kutoka kwa masogora mahiri kufu ya Antoine Griezmann na Kane ambao wanazidi kudhihirisha ukubwa wa uwezo walionao uwanjani.

Mwaka huu, Salah ndiye mchezaji pekee kutoka Afrika aliyetinga ndani ya 10-bora kwa kuambulia nafasi ya sita, na hivyo kuongoza orodha ya wachezaji wanaosakatia klabu za EPL.

Gareth Bale wa Real na timu ya taifa ya Wales alimaliza katika nafasi ya 17 baada ya kupigwa kumbo na Raphael Varane wa Real ambaye pia alitinga 10-bora.

Walioambulia nafasi ya tatu kwenye tuzo za Ballon d’Or nyuma ya Messi na Ronaldo tangu 2008:

2008: Fernando Torres

2009: Xavi Hernandez

2010: Andreas Iniesta

2011: Xavi Hernandez

2012: Andreas Iniesta

2013: Franck Ribery

2014: Manuel Neuer

2015: Neymar Jr

2016: Antoine Griezmann

2017 – Neymar Jr

2018 – Antoine Griezmann