Gavana kuunda chama chake kukabiliana na Raila Pwani
NA LUCY MKANYIKA
GAVANA wa Taita Taveta, Andrew Mwadime, amesema kuwa ataanzisha chama chake cha kisiasa ambapo yeye atakuwa kinara.
Akiongea wakati wa mkutano wa wajumbe wa ODM uliofanyika katika hoteli ya Panlis, Mwatate, Bw Mwadime alisema ataanzisha chama chake baada ya msukosuko aliokabiliana nao katika uchaguzi uliopita, 2022.
Mkutano huo ulihudhuriwa na kinara wa ODM, Raila Odinga, na viongozi wengine wa chama hicho, wakiwemo Naibu Mwenyekiti Wycliffe Oparanya, Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir na Seneta wa Taita Taveta, Jones Mwaruma.
Bw Mwadime alichaguliwa kupitia tiketi ya mgombea huru baada ya juhudi zake za kupata bendera ya ODM wakati wa uchaguzi uliopita kugonga mwamba.
“Nilikuwa na matatizo na chama cha ODM na hiyo ikanipelekea kuwa mgombea huru. Lakini nitakuja kwako tujadiliane kwa kuwa nataka kuwa kinara wa chama na kuwa kinara lazima tuwe na chama cha Mwadime,” akasema.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wakiwemo Bw Oparanya na Bw Mwaruma walisema kuwa viongozi wasioegemea mrengo wowote wa kisiasa hawana ushawishi wowote wa kutetea maslahi ya wananchi.
“Msipigie viongozi wanaosimama kama wagombea huru. Wao ni kama popo, si ndege si mnyama. Ifikapo uchaguzi ujao tuchague viongozi wa chama cha ODM,” akasema Bw Mwaruma.
Bw Oparanya alisema kuwa chama cha ODM ni chama cha kitaifa na kina wafuasi wengi katika kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine ya nchi.
Alisema kuwa kubuniwa kwa vyama vidogo havinufaishi wenyeji na kutoa mfano wa chama cha PAA ambapo hivi majuzi baadhi ya viongozi wake walihamia ODM.
“Wakati wa uchaguzi, vyama vingi vidogovidogo hujitokeza. Wanasema kuwa wanataka chama chao cha kutetea maswala yao. Wale wanaofanya hivyo wanajitafutia maswala yao wenyewe kwa hivyo mjihadhari na watu kama hao,” alisema.