Habari Mseto

Polisi walinipiga na kunishika kwa sababu nilikosa kuwapa hongo, manamba aambia korti

February 1st, 2024 1 min read

NA JOSEPH NDUNDA

MANAMBA wa matatu mwenye umri wa miaka 28 aliyeshtakiwa katika Mahakama ya Makadara kwa kupiga polisi na kukataa kutiwa mbaroni aliambia mahakama kwamba maafisa hao walimpiga na kumtishia kumuondoa eneo alimokuwa kwa kukosa kuwapa hongo.

Derrick Ngetich alishtakiwa kumpiga konstebo wa polisi Charles Muturi kinyume na sheria ambapo anashtakiwa kumuuma kidole kidogo cha mkono wa kulia.

Soma pia Manamba wa matatu mashakani kwa kumuibia na kumbaka mwanamke

Halafu NDIVYO SIVYO: ‘Makanga’ au ‘manamba’ hayafai katika miktadha rasmi

Aidha, anashtakiwa pia kukataa kutiwa mbaroni na Muturi na mwenzake, Patrick Nderitu, wote wanaohudumu katika kituo cha polisi cha Embakasi.

Ngetich anashukiwa kutenda makosa hayo Januari 29, 2024 katika barabara ya North Airport ambapo maafisa hao walikuwa wanamkamata kwa kuning’ingia kwenye gari, ambalo ni kosa la trafiki.

Lakini mshukiwa aliambia Hakimu Mkuu Irene Mugo kwamba anaadhibiwa na maafisa hao kwa kukosa kuwapa hongo, na kwamba walikuwa wameapa kumfunza adabu kwa kumwondoa eneo hilo.

Anadai kwamba maafisa walimuumiza vibaya wakati walipokuwa wanamshika na alimuomba hakimu amuachilie ili aende kutunza mke wake mjamzito aliyesema amekaribia kujifungua.

Ngetich alikabiliwa na wakati mgumu kusimama tisti kizimbani na kutembea kutokana na majeraha aliyosema alipata wakati wa kipigo hicho anachodai polisi walimteremshia.

Bi Mugo alimuachilia kwa dhamana ya Sh5,000 na akamuagiza arudi kwa kituo cha polisi na aripoti kupigwa na polisi hao kwa mkubwa wao ili uchunguzi ufanywe.

Hakimu vilevile aliagiza kwamba mshukiwa apelekwe hospitalini kwa matibabu iwapo atashindwa kupata pesa za dhamana.

Kesi hiyo itatajwa tena Mei 14.

Maafisa hao wa polisi wameorodheshwa kuwa mashahidi pamoja na wenzao waliochunguza kesi hiyo pamoja na daktari aliyewajazia fomu ya P3.