Afya na Jamii

Kula kabeji mara tatu kwa siku husaidia wanaume kupunguza unene

February 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

KULA kabeji mara tatu kwa siku kunapunguza unene kupita kiasi miongoni mwa wanaume, wanasayansi wamebaini.

Katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la BMJ Open, kabeji ambayo imetiwa chumvi , kuchachuka na pia kuongezewa viungo vingine kama vitunguu, husaidia kupunguza unene (obesity).

Msingi wa utafiti huo ni kuwa kabeji ina madini maarufu kama fibre, asidi na vitamini ambayo yanasaidia kupunguza mafuta mengi ndani ya mwili wa mwanamume.

Unene kupita kiasi ni kati ya magonjwa ambayo yanasababisha mauti. Mnamo 2014, serikali ya Kenya ilitoa takwimu ambazo zilionyesha kuwa unene kupita kiasi husababisha asilimia 39 za mauti hapa chini kila mwaka.

Unene kupita kiasi hutokana na kula vyakula ambavyo huongeza nguvu na mafuta mwilini. Vyakula hivyo ni kama ugali, mchele, vile vyenye protini, madini yenye chumvi na pia mafuta.

Utafiti ulionakiliwa kwenye jarida la BMJ Open ulishirikisha wale watu ambao walikula kabeji siku moja na wale ambao walikula chakula hicho mara tatu kwa siku.

Ilibainika waliokula kabeji yenye uchachu mara tatu walipunguza unene huku waliokula kabeji mara moja wakipunguza japo kwa kiwango cha chini.

Kwa upande mwingine, waliokuwa na unene na hawakula kabeji waliendelea kuandamwa na uzani wa juu. Kwa hivyo, utafiti huo uliweka bayana kuwa kula kabeji kwa njia moja au nyingine kunasaidia kupunguza unene ambao unaendelea kuwa kati ya matatizo ya kiafya ya kutisha ulimwenguni.

Hata hivyo, kuna dukuduku kuwa uwepo wa chumvi nyingi katika kabeji ni hatari kwa afya. Lakini, uwepo wa madini ya chumvi (potassium) katika kabeji yenye uchachu husaidia mno.