Wakenya wanaotumia X wamshambulia mwanariadha Kipchoge kwa rambirambi zake kwa Kiptum
FRIDAH OKACHI na GEOFFREY ANENE
WAKENYA kwenye mtandao wa X space almaarufu Twitter wamemkosea adabu mwanariadha mahiri Eliud Kipchoge, wakisisitiza hafai kutoa rambirambi, baada ya ‘kukosa kumpongeza’ Kelvin Kiptum, 24, alipovunja rekodi kwenye mbio za marathon kwa muda wa saa mbili na sekude thelathini na tano.
Mashabiki hao, walimkashifu Eliud Kipchoge, kupakia ujumbe wa rambirambi kwa familia ya Kelvin Kiptum, aliyehusika kwenye ajali na kuaga dunia.
Kwenye ukurasa huo, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kelerwa Salasya alimtaja Bw Kipchoge kuwa mnafiki, akishangazwa jinsi anatoa rambirambi hizo.
“Inahuzunisha, hukumpongeza lakini una mbio ya kutuma ujumbe wa lala salama?” aliuliza Bw Salasya.
Mwingine ni @its_fanuel ambaye alimkashifu mwanariadha huyo mkuu kwa kuchukua muda wa saa kumi kabla ya kuandika ujumbe huo.
Soma pia: Majonzi nyota wa rekodi ya dunia ya marathon, Kiptum akiaga dunia
“Imekuchukua saa kumi kuandika ujumbe huu kwa aya tatu kuhusu rambi rambi zako,” alichangia @its_fanuel.
Kuna wale hawakujali iwapo alimpongeza kupitia vyombo vya habari wakisema kuwa iwapo alimjali mwanariadha mwenza, wakidai hakuandika ujumbe wa pongezi kwenye ukursa wake.
“Haijalishi na mahojiano yaliyofanywa na kituo cha habari, mahojiano hayo ni bure kwa sababu aliulizwa kufanya vile…Ila kwa jumbe za kuomboleza hakuna aliyeuliza…Kwa ufupi, iwapo hakungekuwa na mahojiano, hangemtambua,” alijibu @ Robert_Kipsang wakati wa Pauline Njoroge kumtetea.
Kiptum alifariki pamoja na kocha wake Gervais Hakizimana kutoka Rwanda katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kaptagat mnamo Jumapili usiku.
Gari lake la aina ya Toyota Premio liligonga mti akiwa pia na abiria mwingine Sharon Kosgey aliyekimbizwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya.
Februari 12, Mwanariadha Eliud Kipchoge alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, akisikitishwa na kifo cha Bw Kiptum ambaye alikuwa akiibuka kuwa nyota kwenye mbio za Marathon.
“Nasikitishwa na kifo cha mwanariadha aliyevunja rekodi ya mbio za Marathon na Nyota anayeibuka Kevin Kiptum. Mwanariadha aliyekuwa na maisha ya kuwa mshindi kwa mambo mengi. Natoa rambirambi zangu kwa familia yake changa na mwenyezi Mungu awape faraja wakati huu mgumu,” alipakia Eliud Kipchoge.
Kipchoge alishikilia rekodi ya dunia ya saa 2:01:09 baada ya kushinda Berlin Marathon nchini Ujerumani mnamo Septemba 25, 2022 kabla ya Kiptum kuivunja akitawala Chicago Marathon kwa 2:00:35 mnamo Oktoba 8, 2023.
Licha ya kukosolewa kwa kujikokota kumpongeza Kiptum na pia kutoa rambirambi za pole, Kipchoge ametetewa na sehemu kubwa ya wanaoamini kuwa wanaomlaumu wana chuki naye.
Soma pia: Ubabe uliotarajiwa kati ya Kiptum na Kipchoge katika 42km wazimwa na kifo cha ghafla