Wafanyikazi wa Kaunti ya Nairobi waongezewa mishahara
Na COLLINS OMULO
Krismasi imefika mapema kwa wahudumu 15,000 wa Kaunti ya Nairobi baada ya serikali ya kaunti kuamua kuwaongezea mshahara kuanzia Januari 2019.
Hii ni baada ya usimamizi wa kaunti kuahidi kutekeleza nyongeza ya asilimia 15 iliyoafikiwa kati yake na chama cha wafanyikazi hao (KCGWU), Mei 2017, ambayo ilisajiliwa Septemba mwaka huu.
Naibu Katibu Mkuu wa Kaunti na Msimamizi wa Huduma ya Umma Leboo Morintat alieleza kuwa mkutano wa kamati ya usimamizi katika kaunti ulifanyika Novemba 29, 2018 na kuidhinisha mkataba wa makubaliano (CBA) yaliyosajiliwa Septemba 2018.
“Ni vyema kuelewa kuwa suala la CBA limekuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya uongozi wa Sonko. Kama serikali ya kaunti, tunahitaji kushukuru kwa juhudi za gavana kuwaongezea wafanyikazi wa kaunti mishahara. Kuanzia Januari, wataongezewa mishahara,” aliongeza Bw Morintat katika notisi ya Desemba 13, 2018 kwa wafanyikazi wa kaunti.
Mkataba huo ulisajiliwa katika Mahakama ya Viwanda mbele ya Jaji Nelson Abwodha. Mazungumzo ya nyongeza ya mshahara yamekuwepo tangu 2015.
Mazungumzo hayo yalikubaliwa na kutiwa sahihi na serikali ya kaunti iliyoondoka chini ya usimamizi wa Dkt Evans Kidero.
Chini ya makubaliano hayo, nyongeza ya mishahara ilifaa kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka wa kifedha wa 2017/2018 lakini haikufanyika ingawa serikali ya kaunti ilitenga Sh800 milioni kutekeleza CBA hiyo.