Uasin Gishu kununulia wazee wa vijiji sare kwa Sh10 milioni
WYCLIFF KIPSANG na ONYANGO K’ONYANGO
SERIKALI ya kaunti ya Uasin Gishu itatumia Sh10 milioni kununua sare kwa wazee wa vijiji ikisema hatua hiyo itasaidia wazee hao kutambuliwa kwa urahisi.
Wazee kutoka kaunti ndogo za Soy na Moiben tayari wameanza kupokea sare za rangi ya hudhurungi ilhali wale kutoka Turbo, Kapseret, Kesses na Ainabkoi watapokea zao baadaye.
Wiki jana maafisa wa kaunti walisema wazee 73 kutoka wadi ya Karuna- Meibeki walipokea sare zao katika afisi za chifu za Karandili na Kaplolo.
Mavazi hayo yanatengenezwa katika kiwanda cha Chuo Kikuu cha Moi kinachopatikana ndani ya kiwanda cha kutengeneza nguo cha Rivatex.
Kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti ya Uasin Gishu Josphat Lowoi jana alisema pesa za kugharamia sare hizo tayari zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha wa 2018/2019.
“Seti moja ya sare itagharimu takriban Sh800 na zitagawanywa kwa wazee wote katika kaunti,” said Bw Lowoi.
Serikali hiyo imetetea hatua hiyo ikisema ni njia ya utambulisho. Wazee wetu hutekeleza jukumu kubwa katika jamii na wamekuwa wakilalamika kuwa kila wanapowakamatwa wahalifu nguo zao huraruliwa au kuchafuka,” akasema Bw Wilson Sawe ambaye ni afisa mkuu wa wizara ya Ugatuzi na Utawala.
Hatua ya serikali kuwapa wazee sare imeibua hisia mseto miongoni mwa wakazi.
“Hii hatua ni kitendo cha uhusiano mwema. Pesa hizo zingetumika kufadhili miradi na mipango yenye manufaa kama vile ununuzi wa dawa kwa sababu zahanati nyingi zinakabiliwa na uhaba wa dawa,” akasema Victor Too, mkazi wa eneo bunge la Kapseret.
Lakini Hellen Cherop, mkazi wa Ainabkoi, alipongeza hatua hiyo, akisema sare zitawapa wazee “nguvu na mamlaka zaidi”.
“Kando na sare, wazee hao pia wanapasa kupewa vitambulisho. Hili ni wazo zuri ambalo limeibuliwa na serikali ya kaunti kwa sababu wazee hawa huchangia pakubwa katika mchakato wa kuimarisha usalama,” akasema Bi Cherop.
Mnamo 2014, bunge la seneti liliunda mswada uliolenga kuwatambua wazee kama watumishi wa umma na ambao wanapaswa kupokea mishahara kila mwezi.
Mswada huo ulidhaminiwa na aliyekuwa Seneta wa Pokot Magharibi wakati huo, Profesa John Lonyangapou (sasa Gavana wa kaunti hiyo). Mswada huo ulilenga kuifanyia marekebisho sheria ya Serikali za Kaunti ili wazee wawe wakiajiriwa na Bodi za Huduma wa Umma (PSB) katika kaunti.
Hata hivyo, mswada huo ulikataliwa huku maseneta wakisema kuwa pendekezo hilo ni kinyume cha Katiba.