MakalaSiasa

KRISMASI: Sura mpya za vigogo wa kisiasa wakisherehekea msimu

December 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

KRISMASI ya mwaka huu inatarajiwa kuwa yenye tofauti kubwa kwa viongozi wakuu wa kisiasa ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa mwaka uliopita.

Mabadiliko ya kisiasa yaliyoshuhudiwa nchini mwaka huu yamefanya viongozi wafuatao wawe na hali tofauti ya kimaisha ikilinganishwa na mwaka uliopita kulipokuwa na taharuki baada ya uchaguzi wa urais uliosababisha mgawanyiko katika jamii kitaifa.

RAIS UHURU KENYATTA

RAIS atasherehekea Krismasi akiwa na utulivu ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa mwaka uliopita ambapo uhasama wa kisiasa ulikuwa umetanda nchini baada ya Uchaguzi Mkuu uliofuatwa na marejeleo ya uchaguzi wa urais ambao ulisusiwa na upinzani.

Mwaka huu, Rais Kenyatta ambaye alisafiri Mombasa kwa treni Jumapili, ana kila sababu ya kutabasamu kwani ushirikiano aliofanikiwa kupata na vigogo wa upinzani umempa nafasi bora ya kuchapa kazi bila bughudha.

Tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita ambapo kura za maoni zilionyesha Wakenya wengi wakifa moyo na utawala wake, tafiti za mwaka huu zimepata idadi kubwa ya wananchi wana matumaini hasa kutokana na juhudi zake za kupambana na ufisadi na kuleta amani ya kudumu nchini.

Hata hivyo, angali na mtihani kupunguza gharama ya maisha kwa mwananchi wa kawaida. Kisiasa, rais anashinikizwa na viongozi kadhaa wa Rift Valley atangaze wazi kama atamuunga mkono naibu wake William Ruto kwa urais ifikapo 2022. Vilevile, ngome yake ya Mlima Kenya inataka kujua mrithi atakayeongoza jamii hiyo kisiasa atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi 2022.

 

NAIBU RAIS WILLIAM RUTO

UTAMBULIZI wa naibu rais ulibadilika kutoka ‘Bw Ruto’ hadi ‘Dkt Ruto’ Ijumaa iliyopita alipofuzu na shahada ya uzamifu katika somo la uhusiano wa mimea na mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Tofauti na jinsi Rais Kenyatta alivyopata utulivu kisiasa kufuatia mwafaka wake na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, mambo si shwari kisiasa kwa naibu rais. Mwaka uliopita, Bw Ruto na wafuasi wake wangeapa kwamba Rais Kenyatta na wandani wake wataunga mkono azimio lake la urais 2022.

Hali hii imebadilika sasa kwani wandani wa Bw Ruto wana wasiwasi huenda kuna maelewano ya kisiasa kati ya Rais na Bw Odinga yanayoweza kudhuru azimio hilo lake.

Bw Ruto pia anakumbwa na changamoto ya kuamua kama ataunga mkono marekebisho ya katiba au la, kwani kufikia sasa hana msimamo thabiti kuhusu suala hilo linaloonekana kuungwa mkono na rais. Katika ngome yake ya kisiasa ya Rift Valley, kuna tishio la mgawanyiko wa wapigakura linalotokana na uhasama uliopo kati yake na Seneta wa Baringo Gideon Moi, anayeongoza Chama cha KANU.

 

KIONGOZI WA CHAMA CHA ODM, RAILA ODINGA

HUKU akitarajiwa kujumuika na familia yake bomani mwake katika shamba la Opoda lililo Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga si yule yule aliyetambuliwa wakati wa Krismasi ya mwaka uliopita.

Baada ya muafaka wake na Rais Kenyatta mnamo Machi mwaka huu, maisha yake yamebadilika. Kiongozi huyo wa upinzani mwaka uliopita alipitia masaibu mengi ikiwemo kurushiwa gesi ya kutoa machozi, kurushiwa mawe akiwa kwenye maandamano ya kutetea uchaguzi wa haki na kupoteza wafuasi wake wengi waliodaiwa kuuawa na polisi.

Baada ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, 2017 kufutiliwa mbali, aliamua kutoshiriki kwenye awamu ya pili ya uchaguzi huo aliposisitiza lazima mabadiliko yafanywe kwanza kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), na kumpelekea Rais Kenyatta kushinda. Mwaka huu, Bw Odinga ambaye alipata kazi ya ubalozi wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU), atasherehekea Krismasi akiwa na ulinzi wa serikali mbali na kupewa taadhima kimataifa na katika maeneo yaliyokuwa ya mahasimu wake wakuu wa kisiasa mwaka uliopita.

 

KIONGOZI WA CHAMA CHA WIPER, KALONZO MUSYOKA

BW Musyoka ambaye alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Bw Odinga kwenye uchaguzi wa urais 2017 kupitia Muungano wa NASA, pia amebadili hali yake mwaka huu.

Baada ya kufuata nyayo za Bw Odinga na kukubali kusaidia serikali ya Rais Kenyatta kuleta maendeleo yatakayosaidia wananchi kimaisha, Bw Musyoka alichaguliwa kuwakilisha serikali kama mjumbe maalumu wa amani nchini na kimataifa. Mojawapo ya majukumu yake ni kusimamia Tume ya Kuangalia na Kuchanganua Amani Sudan Kusini.

Sawa na Bw Odinga, serikali ilimrudishia walinzi wake ambao walikuwa wameondolewa wakati kulipokuwa na taharuki za kisiasa mwaka uliopita. Hata hivyo, Bw Musyoka ambaye atasherehekea Krismasi na familia yake nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi, anakumbwa na pingamizi za kisiasa katika ngome yake ya Ukambani kutoka kwa viongozi wanaokosoa uamuzi wake wa kushirikiana na Rais.

 

KIONGOZI WA CHAMA CHA AMANI NATIONAL CONGRESS (ANC), MUSALIA MUDAVADI

KATI ya viongozi wakuu wa NASA, Bw Mudavadi pekee ndiye ameshikilia msimamo wake wa kutoungana na serikali akidai taifa la kidemokrasia halipaswi kuwa bila upinzani wa kuchunguza mienendo ya serikali. Kwa msingi huu, Bw Mudavadi ambaye alikuwa Mombasa wikendi, atasherehekea Krismasi akiwa angali katika upinzani kikamilifu.

Katika ngome yake ya kisiasa eneo la Magharibi, waziri huyo mkuu wa zamani anakumbwa na shinikizo kutoka kwa viongozi wengi wanaompigia debe Naibu Rais William Ruto kwa urais 2022 ajiunge nao. Kwa sasa, Bw Mudavadi anaonekana mpweke kisiasa kwani amekataa kujiunga na vigogo wenzake wa NASA serikalini na vilevile amekataa kuegemea upande wa Bw Ruto akisema hawezi kuungana na mpinzani wake katika uchaguzi wa urais utakaofanyika 2022.