Ndovu 396 waliangamia 2018 – KWS
Na PETER MBURU
JUMLA ya ndovu 396 waliaga dunia kutokana na sababu tofauti mwaka huu, ikilinganishwa na vifo 727 vya wanyama hao ambavyo vilishuhudiwa mwaka uliopita.
Hii ni kulingana na habari iliyotolewa na Shirika la Uhifadhi wa Wanyama Pori (KWS) kuhusu hali ya idadi ya ndovu nchini, hadi Desemba 21 2018.
Shirika hilo liliripoti kuwa vifo hivyo vilitokana na sababu kama uwindaji haramu, magonjwa, ukame, ajali, vifo vya hali za kawaida mbugani na fujo za baina ya binadamu na wanyama pori.
“Kitaifa, nchi ilipoteza ndovu 396 mwaka huu kutokana na sababu tofauti, ikilinganishwa na 727 ambao walifariki 2017. Halii hii inaashiria kupungua kwa asilimia 30 ya jumla ya vifo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita,” sshirika la KWS likasema.
Shirika hilo liliongeza kuwa visa vya uwindaji haramu mwaka huu vilipungua kwa asilimia 50, kutoka visa 80 vilivyorekodiwa 2017, hadi 40. Aidha, KWS ilisema kuwa pembe za wanyama wote walioaga dunia, isipokuwa zile za wale waliouawa na wawindaji haramu, zilipatikana na zinahifadhiwa.
Katika mbuga ya Maasai Mara, jumla ya ndovu 61 waliaga dunia mwaka huu, 23 wakiwa kutokana na vifo vya kawaida, 10 kutokana na fujo za wanyama na binadamu, wanne kufuatia visa vya uwindaji haramu. Hata hivyo, kiini cha vifo vya wanyama 24 hakikufahamika kwani walipopatikana, mizoga yao ilikuwa imeoza kiasi cha kutojulikana kilichosababisha.
Ndovu wawili kutoka mbuga ya Mara aidha walidhibitishwa kufa baada ya kula sumu wakati walitoroka mbugani na kwenda katika mashamba ya watu ambayo yalikuwa yamenyunyiziwa dawa za mimea.
Hata hivyo, kumeripotiwa kuwa na ongezeko la uhasama wa binadamu na wanyama katika mbuga ya Mara, kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, ambayo hayaoani na yale ya uhifadhi wa wanyama pori.
KWS imesema kuwa bado idadi ya ndovu nchini iko imara, kwa sasa ikikisiwa kuwa 35, 000. Idadi hii inaripotiwa kuwa ongezeko la asilimia 119 kwa kipindi cha miaka 29, kutoka ndovu 16,000 mnamo 1989.
“Ndovu katika mbuga ya Mara wameongezeka kutoka 1,000 mnamo 1983 hadi idadi ya sasa 2,493 ambayo ni asilimia 149 ya ongezeko kwa miaka 35,” ujumbe wa KWS ukasema.
Shirika hilo aidha lilisema kuwa ripoti ya mradi uliofanywa na shirika moja kuhusu ndovu katika mbuga ya Mara (MEP) na kunukuliwa katika magazeti kuwa ndovu 26 waliaga dunia baada ya kula sumu haikuwa ya kweli.
“Tangu wakati huo, MEP ilirekebisha ripoti hiyo kwa kutuma ujumbe kwa vyombo vya habari,” KWS ikasema, ikirai umma kutafuta habari kuhusu idadi ama vifo vya wanyama pori kutoka kwake.