Matamshi ya Murathe yaipasua Jubilee
Na WAANDISHI WETU
MATAMSHI ya Naibu Mwenyekiti wa chama tawala cha Jubilee, David Murathe kuwa eneo la Mlima Kenya halitamuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 yamezua joto kali ndani ya chama hicho.
Mnamo Jumatano Bw Murathe alisema hakuna mkataba wowote kati ya Dkt Ruto na jamii ya Mlima Kenya kuhusu uchaguzi wa 2022, matamshi ambayo yalipandisha joto katika kambi ya Naibu Rais jana.
Wandani wa Dkt Ruto na wabunge kutoka Mlima Kenya walimkashifu Bw Murathe na kupuuzilia matamshi yake kama yasiyo na msingi huku wengine wakitaka atimuliwe chamani.
Seneta wa Nandi, Samuel Cherargei na Mbunge wa Soy, Caleb Kositany walimkashifu Bw Murathe wakidai amelipwa na mahasimu wa Dkt Ruto kumchafulia jina.
“Tunajua Murathe ni tapeli wa kisiasa ambaye anatumiwa kumharibia Naibu Rais jina,” akasema Bw Cherargei.
Mbunge wa Kuresoi Kusini, Joseph Tonui na mfanyabiashara Shadrack Koskei nao walimkashifu Bw Murathe na kumtaka kuomba msamaha kufuatia matamshi yake.
“Matamshi ya Bw Murathe hayakufaa kwani Dkt Ruto ndiye aliyeongoza kampeni za Rais Kenyatta katika chaguzi za 2002, 2013 na 2017. Tayari ana uungwaji mkono kote nchini,” akasema Bw Koskei.
Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya pia walimkashifu Bw Murathe na kutaka avuliwe mamlaka katika Jubilee. Viongozi hao pia walimtaka Rais Kenyatta kujitokeza kukanusha matamshi ya Bw Murathe.
Wabunge Gichunge Kabeabea (Tigania Mashariki), Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini) walisisitiza kuwa eneo hilo lilifanya uamuzi wa kuunga mkono Dkt Ruto katika azma yake ya urais 2022.
“Uhuru anafaa kuitisha uchaguzi wa chama mara moja ili Murathe aondolewe kwani analeta utengano katika chama,” akasema Bw Dawood.
Katika Kaunti ya Nyeri, Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alimkashifu Bw Murathe akisema matamshi yake hayakuwakilisha eneo la Mlima Kenya, msimamo ulioungwa mkono na Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Kirinyaga, Muriithi wa Kang’ara na Mbunge wa Mukurweini, Anthony Kiai waliotaja matamshi ya Bw Murathe kuwa yake binafsi.
Wabunge Patrick Munene wa Chuka/Igambang’ombe na Gitonga Murugara wa Tharaka nao walisema wabunge wa Jubilee hawajawahi kujadili kuhusu mambo aliyozungumzia Bw Murathe.
Lakini Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau waliunga mkono matamshi ya Bw Murathe.