Mshubiri wa Krismasi kwa familia baada ya mauti kubisha
Na LUCY MKANYIKA na GERALD BWISA
FAMILIA mbili katika kaunti za Taita Taveta na Trans Nzoia zinaomboleza kufuatia mikasa wakati wa sherehe za Krismasi.
Katika kisa cha Taita Taveta, familia ya mtoto wa miaka minane inaomboleza kifo chake baada ya mwili wake kupatikana katika bwawa la hoteli moja.
Polisi wa eneo hilo wanachunguza kifo hicho ambapo mwili wa mtoto huyo ulipatikana ukielea juu ya maji baada ya kutoweka walipozuru hoteli ya Shasha Camp kusherehekea krismasi.
OCPD wa Mwatate Monica Kimani alisema kuwa wazazi wa marehemu walipiga ripoti kuwa mwanao alikuwa amepotea baada ya kumtafuta hadi mwendo wa saa moja usiku.
“Baada ya kumtafuta kila mahali walipata nguo zake karibu na bwawa hilo. Hata hivyo hawakumuona ndani ya bwawa,” akasema Bi Kimani.
OCPD huyo alieleza kuwa mwili wa mtoto huyo ulipatikana ukielea katika bwawa hilo kesho yake.
Alisema kuwa wameanzisha uchunguzi kubaini ikiwa mtoto huyo aliuawa na kisha mwili wake kutupwa hapo.
“Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Moi mjini Voi ukingoja kufanyiwa upasuaji ili kufahamu kiini cha kifo chake,” akasema.
Meneja wa hoteli hiyo Bw Allen Mwazala alisema kuwa walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa amekatazwa na wazazi wake kuogelea.
“Huenda ikawa alitoroka wazazi wake ili kuogelea,” akasema.
Hata hivyo alisema kuwa hoteli hiyo haina wahudumu wa kuzuia visa kama hivyo katika bwawa hilo.
“Huwa tunawatahadharisha wateja wetu wawe makini wanapoogelea,” akasema.
Katika kisa kingine, mvulana wa miaka 17 alifariki Jumatano kwenye bwawa la kuogelea katika mkahawa wa Le-Voyage Resort, Kaunti ya Trans Nzoia.
Mwathiriwa, aliyetambuliwa kama David Ndegwa, ni mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Upili ya Kibomet na alifariki wakati akiogelea na rafikize katika bwawa hilo.
Meneja wa hoteli hiyo Michael Werunga aliiambia Taifa Leo kwamba kulikuwa na watu wengi bwawani, hivyo ilikuwa vigumu sana kubaini mara moja mkasa huo ulipotokea.
Mkuu wa Polisi wa Trans Nzoia Magharibi, Jackson Mwenga alithibitisha kisa hicho.