• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Wakulima washtuka Rais hajapata ripoti ya mahindi

Wakulima washtuka Rais hajapata ripoti ya mahindi

Na ONYANGO K’ONYANGO

WAKULIMA na viongozi wa eneo la North Rift wameilaumu kamati iliyoteuliwa kuchunguza kashfa ya mahindi kwa kutowasilisha ripoti yao kwa Rais Uhuru Kenyatta kabla ya mwaka mpya ndipo wajue hatma yao kabla ya shule kufunguliwa Januari 3, 2019.

Wakulima hao waliozugumza na Taifa Leo waliwakashfu Magavana Jackson Mandago (Uasin Gishu) na Patrick Khaemba (Trans-Nzoia) kwa kuchelea kuikabili Serikali kuyanunua mahindi kwa bei ya juu ikizingatiwa kuwa gharama ya kuyakuza iko juu.

Wanazaraa hao walisema hayo baada ya Rais Kenyatta kusema Ijumaa kuwa hajapokea ripoti ya mahindi licha ya tangazo la Bw Mandago, Desemba 20, 2018 kwamba itapelekewa Rais Desemba 24, 2018.

“Tulishangazwa na matamshi ya Rais Kenyatta kwamba hajakabidhiwa ripoti hiyo na kamati inayochunguza shida inayokumba kilimo cha mahindi. Ni wazi kwamba magavana hawa wawili wanajihusisha na siasa za kujifaidi wenyewe na wala sio maslahi ya waklima. Wamekuwa katika mstari wa mbele kuhimiza wakulima washiriki kilimo cha mimea mingine badala ya kuchangamkia jinsi wakulima watakavyolipwa Sh2.1 bilioni wanazodai,” alisema Bw Kipkorir Menjo, mkurugenzi wa chama cha wakulima (KFA).

Akizugumza kwa simu Bw Menjo aliongeza, “Wakulima wengi wamechanganyikiwa kwa sababu wanayategemea mahindi kulipia watoto wao karo za shule.Shule zinafungunguliwa wiki hii na maghala ya kuhifadhi mahindi ya halmashauri ya nafaka na mazao (NCPB) yatafunguliwa kati kati ya Januari 2019 badala ya Desemba 2018. Kucheleweshwa kufunguliwa kwa maghala haya kunamaanisha wakulima watakabiliwa na wakati mgumu kulipa karo za shule. Tulitazamia viongozi wetu tuliowachagua katika kamati hiyo kutetea kufunguliwa kwa maghala mapema.

Wakuzaji hawa wa nafaka walitoa wito kwa hazina ya kuhakikisha kuna chakula cha kutosha (SFRTF) ifutiliwe mbali wakidai haina uongozi unaozingatia maslahi ya wakulima wa zao la mahindi.

“SFRTF imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha haki za wakulima zimepewa kipau mbele. Kule kukubalia gunia la mahindi ya kilo 90 kuuzwa kwa Sh2,300 ni hakikisho kuwa hazina hiyo haitilii maanani haki ya mkulima na badala yake inatetea magenge ambayo yameingilia kilimo cha mahindi ,” alisema Menjo.

Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei alisema bodi hiyo ya SFRTF inayoongozwa na waziri wa zamani, Dkt Noah Wekesa inajaribu juu chini kushinikiza yapo makundi yanayodai serikali itanunua magunia 2.5 milioni ya mahindi.

You can share this post!

2019: Mgomo kuanza Alhamisi huku Knut ikikaza kamba

Familia yamlilia Uhuru aingilie kati Tanzania imwachilie...

adminleo