• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
NMG yawatuza wauzaji wa magazeti

NMG yawatuza wauzaji wa magazeti

NA RICHARD MAOSI

Kampuni ya Nation Media Group kitengo cha magazeti  Jumatatu iliwatuza wauzaji magazeti kote nchini kwa kuwatunuku zawadi ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Shindano hili lililopatiwa jina la Chrismas Comes Early for our Vendors liliwaleta pamoja wauzaji kutoka  kaunti 47 kote nchini,waliofanya vizuri katika mauzo yao kati ya Disemba 10 hadi 18.

Siku ya Jumamosi gazeti la Daily Nation lilichapisha majina yao gazetini ili kuwapa motisha kutokana na juhudi zao za kila siku sokoni.

Hatua hii inapania kuwatia shime wauzaji kote nchini wanaojitolea kwa hali na mali kuhakikisha magazeti ya Daily Nation, Taifa Leo, Business Daily, Mwanaspoti, na The East African yamevutia wasomaji.

Kulingana na mkurugenzi wa mauzo katika bonde la ufa Bw Timothy Siran, hii ni mojawapo ya njia za kurudisha mkono katika jamii kutokana na utendakazi mzuri mwaka mzima licha ya kuwepo kwa majarida mengi.

Aidha wauzaji hawakuwa na budi ila kuonyesha furaha yao walipopokezwa tishati ta zenye nembo za Nation, kofia na kitita taslimu ambacho hakikuwekwa wazi.

Bw Alex Ambagwa, mojawapo ya wauzaji walioibuka kidedea katika uuzaji magazeti nchini. Picha/ Richard Maosi

John Omboka alianza kuuza magazeti miaka ya 70 na ndiyo njia ya kipekee inayompatia riziki. Anasema ameshuhudia matukio muhimu nchini tangu uongozi wa Kenyatta mpaka sasa na anawahimiza hususan vijana kukumbatia desturi ya kusoma ili kupanua mawazo yao.

“Elimu haina mwisho pia ni kubwa kushinda bahari kadri binadamu anavyoishi ndivyo anavyozidi kujifunza kutokana na changamoto za maisha. Kumbukumbu hizi zote zinaweza kuhifadhiwa katika matini yaliyoandikwa,” alisema.

Katika pitapita zetu katika barabara za mjini Nakuru, Taifa Leo Dijitali  ilikutana na Brian Mwangi, muuzaji wa haiba kubwa. Anasema wateja wake wengi wanatoka eneo la Section 58, Mawanga na Kiamunyi.

Anasimulia kuwa siri kubwa ya kuimarisha mauzo ni pale muuzaji anachukuwa wakati wake mkubwa kumrai msomaji na kumshawishi .

Awe jasiri na akubali hali halisi na kufahamu fika mauzo yanaweza kupanda msimu fulani na pia kuteremka kulingana na mahitaji ya soko.

“Wasomaji wengi hupendelea kujikita katika matukio yanayohusu eneo lao,” alisema Mwangi.

George Okoko Ouma anaeleza tangu aanze kuuza gazeti amefanikiwa kujitosheleza kimaisha kutokana na kipato anachovuna kila mwezi .Amejiongezea mtaji na kujiendeleza.

Alitumia faida inayotokana na uuzaji magazeti kulipa mahari na kuwasomesha watoto wake, bali na kujinunulia na kujenga nyumba katika ploti yake..

You can share this post!

Mashabiki waitaka Ingwe iwagware Rangers kukomesha matokeo...

Purukushani harusini kidosho akidai kuwa mke wa bwana harusi

adminleo