Makala

2018: Habari 10 zilizovutia wasomaji katika tovuti ya Taifa Leo

January 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 4

NA FAUSTINE NGILA

LICHA ya mwaka wa 2018 kukumbwa na mawimbi ya sakata nyingi za ufisadi, tukio la kiongozi wa ODM kujiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’, Dkt Miguna kufurushwa nje ya nchi na hatua ya maridhiano ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, Wakenya walipendekezwa na habari tofauti, kama inavyoashiriwa na orodha ifuatayo.

 

  1. Kijana aliyetoroka Al Shabaab asimulia maisha yalivyokuwa akiwa gaidi

Hii ilikuwa simulizi baada ya Taifa Leo kukutana na kijana wa miaka 29 katika kaunti ya Kwale aliyerudi nchini 2015 baada ya kuchoshwa na kuwa mtumwa wa Al Shabaab.

Alialikwa na binamu yake mjini Lamu kwa ahadi kuwa angepata kazi nzuri. Aliishi kwa kwake kwa miezi mitatu kisha akamtambulisha kwa vijana wengine watatu kisha wakapewa Sh10,000 kila mmoja. Aliwahadaa wakaingia gari la kibinafsi wapelekwe mahala ambapo wangeanza kufanya kazi ya mshahara wa Sh40,000 kwa mwezi.

Lakini walijipata kwenye kambi iliyokuwa na vijana wapatao 200. Hapo ndipo alipong’amua kuwa alikuwa ndani ya kambi ya Al Shabaab nchini Somalia. Humo kambini walianza kupokea mafunzo ya kijeshi ambayo yalikuwa yachukue miaka miwili. Baadaye wangetumwa uwanja wa vita kupigana.

Mafunzo yalikuwa makali sana. Tulikuwa wakiamka saa kumi alfajiri ambapo walishiriki mafunzo na mazoezi hadi saa kumi na moja jioni.

Mafunzo yalihusisha jinsi ya kutumia silaha tofauti kama bunduki, gurunedi miongoni mwa nyingine. Pia walibebeshwa magunia mazito yaliyojaa mchanga. Ilikuwa ni lazima ushiriki mafunzo upende usipende.

Aligombana na kamanda na akapanga na Mkenya mwingine jinsi wangehepa. Walitoroka usiku wakiogopa kuuawa na wenzao wa Al Shabaab.

Baada ya kutembea kwa siku mbili msituni walipatana na mzee ambaye aliwasaidia kufika Mandera. Kisha waliingia lori lililotupeleka Garissa.

Simulizi hii ilivutia wasomaji wengi zaidi kwa kuwa walitaka kuelewa kuhusu mafunzo ya Al Shabaab na jinsi walifika Kenya.

 

  1. Kioja demu kuangua kilio baada ya bosi wake kukataa kumbusu

Hii ilikuwa mojawapo ya habari za ucheshi zinazochapishwa kwenye sehemu ya Dondoo kwenye gazeti.

Kioja hicho kilitokea mjini Kiambere ambapo ‘slay queen’ mmoja alishangaza wapangaji alipoanza kulia akimlaumu mdosi wake kwa kumnyima busu.

Kitendo hicho kiliwafanya wafanyakazi wenzake kubaini kwamba demu huyo alikuwa na uhusiano wa mapenzi na mdosi ambaye ana mke na watoto.

Yasemekana uhusiano huo ulikuwa umeanza kuingia baridi na demu akamwendea mdosi na kumtaka ambusu.

Wasomaji wa tovuti yetu mwaka uliopita walikita kambi kwa habari za Dondoo huku sehemu hiyo ikiibuka nambari tatu kwa vitengo vya habari vilivyosomwa zaidi.

 

  1. Zambia kuwasukuma jela watakaonaswa wakiwa na ‘Samantha’

Habari hii ilivutia hisia za wasomaji wakati ambao vinyago vya visura vilikuwa vinaundwa kwa wingi duniani na hata kufika Kenya na Zambia.

Lakini serikali ya Zambia ikaanzisha msako mkali dhidi ya madoli hayo ya mahaba na kuonya kuwa watakaopatikana nayo wangeadhibiwa kwa kusukumwa gerezani.

Hatua hiyo ilipelekea suala la madoli ya mahaba kugongwa vichwa vya habari kwa mwezi mzima wa Februari na kuibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.

Wasomaji walishangaa ni vipi mwanamume mwenye akili zake timamu atanunua kinyago badala ya kusaka urafiki na msichana binadamu.

 

  1. Riba ya ‘Okoa Jahazi’ ya Safaricom ni haramu, wananchi waambia mahakama

Wakenya wengi husukumwa na makali ya gharama ya juu ya maisha kuchukua mkopo wa muda wa maongezi kutoka kwa kampuni ya Safaricom.

Hiyo ilichochea Wakenya wawili kuishataki Safaricom kuhusiana na huduma yake ya ‘Okoa Jahazi’ ambayo walisema hutozwa riba waliyodai ni haramu.

Ashford Koome na Eric Kithinji walidai kuwa kampuni hiyo haijapewa leseni ya kutoa huduma za benki, hivyo, riba wanayotoza huduma hiyo ilikuwa haramu.

Hata hivyo, kwa kujitetea, kampuni hiyo ilisema hiyo ni ada na sio riba kama walivyodai, kwa kuwa imeidhinishwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA).

 

  1. Miguna Miguna: Raila ndiye aliniambia Jubilee ilimpa Magaya Sh30 milioni

WAKILI mbishi Miguna Miguna aliedai kwamba kinara wa ODM, Raila Odinga, alimweleza binafsi kwamba Bw Norman Magaya, alipokea Sh30 milioni kutoka kwa chama cha Jubilee.

Akihojiwa na kituo cha runinga cha TRT World jijini Toronto, Canada, Bw Miguna alikanusha madai kwamba alikuwa anampiga vita Bw Odinga.

“Ni kweli Bw Magaya alipokea Sh30 milioni kutoka kwa Jubilee ndipo aondoe kesi ya kupinga ushindi wa gavana wa Nairobi. Raila Odinga mwenyewe alinifahamisha hayo,” alidai Bw Miguna.

 

  1. Tutajiapisha kama Raila Odinga, upinzani nchini Venezuela wasema

Wanasiasa wa upinzani nchini Venezuela walitangaza kuwa wangemuiga Bw Raila Odinga kwa kuapisha mwaniaji wao ikiwa Rais Nicolas Maduro angeiba kura katika uchaguzi wa mwaka uliopita.

Mwanaharakati wa kisiasa wa upinzani David Smolansky alisema kuwa Bw Odinga alikuwa kielelezo kwao kwa kujiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ baada ya kuwepo kwa udanganyifu wa kura.

Bw Smolansky aliyekuwa akizungumza katika mahojiano na kipindi cha HARDtalk katika runinga ya BBC, alisema Upinzani pia ungesusia uchaguzi uliopangwa kufanyika Aprili 22, 2018.

 

  1. BI TAIFA JULAI 28, 2018

Wasomaji wetu pia hupendezwa na ukurasa wa tatu wa gazeti ambapo picha za wasichana warembo kutoka maeneo tofauti ya nchi huchapishwa. Wasomaji walipendezwa na picha za Bi Taifa kwa jina Cecilia Rioba aliyekuwa na miaka 25 mwaka 2018.

 

  1. BOBI WINE: Shinikizo kwa Museveni aachilie huru msanii zazidi

Wasomaji pia walitazama video ya maandamano yaliyofanyika Nairobi, huku Wakenya wakimshinikiza Rais Yoweri Museveni wa Uganda amwachilie huru Bobi Wine. Ilishangaza maandamano haya kufanyika Kenya maanake Bobi Wine si Mkenya.

 

  1. Kwaheri Volkswagen Beatle

Wapenzi wa magari ya Volkwagen walishtuka baada ya kampuni hiyo kutangaza kukomesha utengenezaji wa gari aina ya Beatle ambalo lilipata umaarufu ulimwenguni miaka ya zamani, na kusema itakuwa ikiunda magari ya kielektroniki.

 

  1. Waziri Echesa ashauriwa arudi shuleni kunoa maarifa

Waziri wa Michezo na Turathi Bw Rashid Echesa Muhamed alishauriwa kutumia nafasi yake ya uwaziri kurejea shule kujiendeleza kimasomo.

Lakini kiongozi wa wengi Aden Duale alisema uhitimu wa kimasomo siyo hitaji kuu kuliko uwezo wa mtu kutekeleza majukumu ya uwaziri.

“Kazi ya uwaziri haina uhusiano wowote na shahada za digrii au chuo kikuu ambacho mtu alisomea bali uwezo wake wa kutekeleza majukumu aliyopewa,” akasema Bw Duale.