Miradi iliyoidhinishwa kabla ya mafuriko sasa kukaguliwa upya
NA WINNIE ONYANDO
GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amebuni kikosi kipya kilichopewa jukumu la kukagua upya miradi ya ujenzi iliyoidhinishwa kwa muda wa miaka miwili iliyopita.
Kulingana na gavana huyo, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa miradi au majengo hayo yanakidhi viwango vilivyowekwa.
“Tayari Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi kupitia kwa afisi ya kaimu Katibu wa Kaunti imewaandikia wadau mbalimbali kuwaomba kuwasilisha majina ya wataalamu na wawakilishi ambao sasa watakuwa sehemu ya jopokazi la ukaguzi huo,” akasema Gavana Sakaja kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Wanachama wa timu hiyo ya ukaguzi watakutana mnamo Juni 12, 2024, ili kuanza ukaguzi huo.
Wana siku 60 za kukamilisha kazi hiyo ya ukaguzi na kuwasilisha ripoti kwa ajili ya utekelezaji.
Kando na hayo, gavana huyo pia amerejesha uidhinishaji wa mipangilio ya ujenzi iliyokuwa imesitishwa wakati ghorofa zilikuwa zinaanguka kukiwa na mafuriko jijini.
Gavana alikuwa amesitisha uidhinishaji mpya wa mipangilio ya ujenzi katika maeneo ya ujenzi wakati wa mvua kubwa na mafuriko yaliyokuwa yakishuhudiwa.