Jamvi La Siasa

Pigo KK wabunge wake nao wakipinga Mswada wa Fedha

June 8th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

HUENDA muungano wa Kenya Kwanza ukakumbwa na wakati mgumu kufanikisha kuupitisha Mswada wa Fedha wa 2024 Bungeni baada ya baadhi ya wabunge wa mrengo huo kuahidi kuupinga.

Wabunge hao wameamua kukaidi msimamo wa mrengo huo wa kuunga mkono na kujihusisha na msimamo wa raia kwamba mapendekezo ya kuongezwa kwa ushuru kwa bidhaa na huduma za kimsingi yatawaumiza zaidi raia badala ya kuwaokoa kutoka lindi la shida.

Kando na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, ambaye amekuwa akipinga nyongeza ya ushuru tangu mwaka jana, wabunge David Ochieng (Ugenya) na Dancan Mathenge (Nyeri Mjini) sasa wamejitokeza waziwazi kupinga mswada huo tata.

Bw Ochieng’, ambaye pia ndiye kiongozi wa Chama cha Movement for Democratic Growth (MDG), ameelezea hofu kuwa mswada huo unaweza kuchochea mapinduzi nchini ikiwa utapitishwa ulivyo pasina kufanyiwa marekebisho kuondoa mzigo wa ushuru unaobebeshwa wananchi.

“Tunachochea mapinduzi, hauwezi kumtoza mfanyakazi ushuru kiasi kwamba habaki chochote baada ya kufanyakazi kwa mwezi mmoja. Nitapiga kura ya kupinga mapendekezo yote kwenye mswada huo yanayolenga kuongeza ushuru kupitia kiasi,” Bw Ochieng akasema Jumanne kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.

Ni mbaya

“Ningependa kuwashauri walioandaa mswada huu, na ninajua kwamba wananisikiliza na kunitazama, kwamba mswada wa fedha wa mwaka huu ni mbaya na unapasa kuondolewa,” akaongeza.

Bw Ochieng’ alitoa mfano wa pendekezo la kuanzishwa kwa ushuru wa magari wa kima cha asilimia 2.5 ya thamani ya gari lenyewe, ushuru wa VAT wa asilimia 16 kwa mkato, ushuru wa asilimia 20 unapendekezwa kutozwa mafuta ya kupikia, akisema zitachangia kuongezeka kwa gharama ya maisha.

“Tunafaa kuongeza ushuru kwa bidhaa za starehe bali sio kwa bidhaa za kimsingi,” akaeleza.

Chama cha MDG ni miongoni mwa vyama vilivyogura muungano wa Azimio na kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Bw Ochieng’ amekuwa mtetezi sugu wa Rais William Ruto na sera yake ya kuchochea ukuaji wa kiuchumi kuanzia ngazi za mashinani, maarufu kwa kimombo kama “Bottom-Up Economic Transformation-BETA”

Kwa upande mwingine, Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili bungeni, amekuwa mkosoaji mkubwa kinara wa Azimio Raila Odinga na chama cha ODM, chenye ushawishi mkubwa katika eneo bunge analiwakilisha la Ugenya.

Kinaya ni kwamba, licha ya umaarufu huo, Bw Ochieng’ amefaulu kuwabwaga wagombeaji wa ODM katika eneo bunge hilo mara mbili, 2017 na 2022.

Kwa upande wake, Bw Mathenge, ameapa kukaidi msimamo wa Kenya Kwanza na kupinga mswada huo wa Fedha wa 2024 utakapopigia kura bungeni baadaye mwezi huu.

“Msimamo wangu binafsi kama mwakilishi wa watu wa Nyeri Mjini ni kwamba mswada huu utawaumizia ukipitishwa ulivyo. Kwa mfano huu ushuru magari unapasa kupunguzwa kabisa au uondolewe kabisa,” anasema.

“Sababu ni kwamba huu ushuru wa kima cha asilimia 2.5 utachangia kuongezeka kwa gharama ya uchukuzi na wakulima raia wa kawaida, wakiwemo wakulima ndio wataathiri. Ikiwa ni lazima serikali itoze ushuru basi upunguzwe hadi kima cha asilimia 0.5,” anaongeza Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili.

Baadhi ya wabunge wengine wa Kenya Kwanza tuliozungumza nao waliukataa mswada huo lakini wakaomba tusiwataje majina kwa hofu ya kumkwaza Rais Ruto.

Kulingana na Bw Martin Andati, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, misukosuko inayotokota ndani ya chama cha UDA pia huenda ikachangia wabunge wengine kupinga mswada huo wa fedha.