Habari za Kitaifa

Bei ya unga kuendelea kushuka nchini


BEI ya unga wa ugali inatarajiwa kuendelea kushuka kutokana na mavuno ya zao la msimu huu na kuwasili kwa mazao ya bei nafuu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Wateja ndio watakaonufaika na kushuka kwa kasi kwa bei ya mahindi kutoka Sh4,600 hadi Sh2,500 kwa gunia la kilo 90 katika maeneo ya North Rift katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na mavuno ya msimu huu na kuwasili kwa mazao ya gharama nafuu kutoka Uganda.

Bei ya bidhaa hiyo imeshuka kutoka Sh5,200 hadi Sh3,400 mjini Kisumu na Sh3,200 mjini Nakuru kutokana na kuongezeka kwa usambazaji wa mazao sokoni na mavuno ya mazao mbadala.

“Bei ya mahindi inatarajiwa kupungua huku mavuno ya mazao mbadala ikiongezeka hasa katika maeneo ya eneo la Magharibi mwa Kenya,” alisema Moses Kiptoo, mfanyabiashara wa mahindi Eldoret.

Wasagaji mahindi wamepunguza shughuli zao ili kuwaepusha na hasara zaidi kutokana na msongamano wa soko ambao umechangiwa na kushuka kwa bei ya mahindi na kuwanufaisha watumiaji ambao watanunua bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

“Tunachoshuhudia ni kwamba wasagaji mahindi, waendeshaji wakubwa na wadogo wamepunguza ununuzi kutokana na kupungua kwa mahitaji ya unga,” David Maina, msagaji mahindi Eldoret alisema.

Tahadhari ya kushuka zaidi kwa mahindi

Wasagaji mahindi wametahadharisha kuhusu kushuka zaidi kwa bei ya mahindi kufuatia mavuno ya mazao ya muda mfupi na kuwasili kwa mazao ya bei nafuu kutoka nchi wanachama wa EAC, na hivyo kusema kuwa ni hatari kwa wakulima ambao watapata hasara.

“Baadhi ya watumiaji sasa wanakula vyakula mbadala jambo ambalo limewaathiri baadhi ya watu wanaosaga mahindi,” akasema Simon Mutai, mmoja wa wanaosaga mahindi.

Bei ya unga wa mahindi imepungua kutoka Sh160 hadi Sh120 kwa pakiti ya kilo 2 lakini bei hiyo inatarajiwa kupungua zaidi kufuatia kuwasili kwa bidhaa za bei nafuu.

Hii itawaathiri zaidi wakulima wa mahindi katika eneo la North Rift ambao wamekuwa wakihifadhi mazao hayo wakitarajia bei ipande.

“Tulijua kuwa bei ya mahindi ingepanda kama ilivyokuwa hapo nyuma ambapo kilo 90 ya bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa Sh7,200 ila mambo yamebadilika msimu huu. Hii ni hasara kubwa kwetu,” akasema Jackson Rotich kutoka Ndalat kaunti ya Nandi.

Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) imekuwa ikinunua bidhaa hilyo kwa Sh4,000 kwa kila mfuko wa Kilo 90.

Bohari ya Eldoret NCPB kwa mfano imekuwa ikipokea kati ya gunia 5,000 hadi 8000 za mahindi kila siku huku wakulima wakitarajia kufaidika kutokana na bei bora na malipo ya haraka ya mazao hayo.