Habari MsetoSiasa

Gavana Nanok kuwaadhibu wafanyakazi wazembe wanaokwama mitandaoni

January 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY LUTTA

GAVANA wa Turkana, Josphat Nanok, ametishia kuwaadhibu wafanyakazi wa kaunti wanaopoteza wakati katika mitandao ya kijamii na kuzembea kazini.

Alionya kuwa serikali yake haitaongeza muda wa kandarasi za kazi za wafanyakazi ambao hawatatimiza majukumu yao.

Bw Nanok alisema baadhi ya wafanyakazi wa Kaunti hutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii wakijadili siasa badala ya kuzingatia kazi yao.

Alisema wengine huwa wanafuja mali ya umma badala ya kufanya kazi.

“Kwa sasa, serikali yangu inaziba mianya yote kuhakikisha pesa za umma zitatumiwa vyema. Sio kwamba Kaunti haina pesa, mfumo wa fedha umelindwa vyema,” alisema.

Bw Nanok alisema kwa sasa, kupitia mfumo wa malipo wa serikali (Ifmis) serikali yake imekoma kutumia hundi kulipa wanakandarasi ili kuzima wizi wa pesa.

Gavana Nanok alikuwa akizungumza Alhamisi katika makao makuu ya serikali ya Kaunti mjini Lodwar wakati wa kuapishwa kwa maafisa wanne.

Maafisa hao ni Askofu Joshua Lemuya (Kilimo), Bi Pauline Akai Lokuruka (Utalii, utamaduni na rasilmali),Abdullahi Yusuf Mohammed ( Mipango) na Rosemary Nchinyei ( biashara na masuala ya vijana).

Bw Nanok aliambia kila mfanyakazi wa serikali ya kaunti yake kuzingatia kazi yake kwa makini akisema hatawajibikia makosa na uzembe wao.

Kila mfanyakazi hasa mawaziri, maafisa wakuu na wakurugenzi lazima apate habari za miradi iliyo chini ya idara yake. Kwa nini niwe nikieleza mradi unavyoendelea?” aliuliza.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na seneta Malachy Ekal, wabunge Joyce Emanikor ( mwakilishi wa wanawake), James Lomenen ( Turkana Kusini), John Lodepe (Turkana Kati), Daniel Epuyo (Turkana Magharibi) na Mohammed Ali Lokiru (Turkana Mashariki) ambao waliahidi kuhakikisha miradi ya kaunti itafaulu.

Bw Lomenen aliahidi Gavana Nanok kuhakikisha miradi iliyokwama imekamilishwa kwanza na kukabidhiwa umma.

“Wale ambao uliteua katika serikali yako na hawakuheshimu kwa kuhakikisha manifesto yako imetekelezwa huku wakipora mali ya umma wanafaa kuchukuliwa hatua,” alisema mbunge huyo.

Bw Lomorukai alimtaka afisa anayesimamia kilimo kuhakikisha kwamba kuna pesa za kutosha kufadhili miradi ya kunyunyuzia mashamba maji ili kutatua shida ya uhaba wa chakula katika kaunti hiyo.