Serikali kudhibiti bei ya dawa madukani
NA ANGELA OKETCH
SERIKALI inatathmini uwezekano wa kuanza kudhibiti bei ya dawa ili kuhakikisha dawa haziuzwi nchini kwa bei ghali kuliko bei inayofaa katika kiwango cha kimataifa.
Utathmini huo unajiri baada ya Halmashauri ya Kusambaza Dawa nchini (Kemsa) kushusha bei za dawa kwa asilimia 8 ikilinganishwa na bei ya kimataifa kutoka ile ya awali ya asilimia 35.
Hatua hiyo inatokea baada ya utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya kufichua kwamba baadhi ya dawa zilikuwa zikiuzwa kwa zaidi ya mara mbili ya bei ya kimataifa au bei ya juu isiyofaa.
Kulingana na Waziri wa Afya, Sicily Kariuki, hatua hiyo itasaidia juhudi za taifa kufikia usawa wa afya kwa raia wote kufikia mwaka wa 2022.
Bi Kariuki anasisitiza kwamba ukosefu wa asasi maalum ya kudhibiti bei za dawa ni kikwazo kikuu kwa utimizaji wa ajenda hiyo.
“Hatujawahi kubuni asasi ya kudhibiti bei za dawa na bidhaa nyingine za mtibabu. Hii imepelekea wafanyabiashara kuuza dawa kwa jinsi watakavyo,” akasema Bi Kariuki.
Waziri huyo alisema wizara yake imefikia makubaliano na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu bei za wastani za dawa zitakazotumika nchini.
“Bei ya juu ya dawa ni mojawapo ya sababu zinazochangia ukosefu wake na huwa mzigo mkubwa sana kwa wagonjwa wanaozihitaji,” akaongeza Bi Kariuki.