Washukiwa watatu wa maandamano wazirai kortini kwa sababu ya njaa
WASHUKIWA watatu kati ya 185 waliokamatwa Jumanne, Julai 2, 2024 kwa kushiriki maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 walizirai katika Mahakama ya Milimani Jumatano usiku.
Ilibidi hakimu mwandamizi Wandia Nyamu aamuru polisi watafute maziwa kuwapa washukiwa hao “wasiage dunia ndani na ukumbi wa mahakama.”
“Patieni watoto hao maziwa. Chukueni maziwa kutoka kwa afisi yangu muwape watoto hawa,” Bi Nyamu aliamuru maafisa wa polisi waliokuwa wanashika doria kortini.
Waandamanaji hao wa umri kati ya miaka 16-17 walimweleza hakimu tangu walipotiwa nguvuni hawakupewa chakula.
“Mheshimiwa twafa njaa. Hatukupewa maji, chai au mkate ama chakula kinginge kile tangu tulipokamatwa na polisi,” mshukiwa mmoja aliungama huku sauti yake ikififia kisha akaanguka nusra akate roho.
Watatu hao walikuwa wadhaifu hata kusimama ilikuwa shida.
Kuona washukiwa hao wamezidiwa na njaa hakimu aliamuru watolewe nje ya ukumbi wa mahakama wapewe maziwa na huduma ya kwanza.
Polisi waliwatoa washukiwa hao nje na kuwapa maziwa.
Baada ya nusu saa washukiwa hao walirudi ukumbini kesi ilipokuwa inasikizwa na kuomba waachiliwe.
Mbali na watatu hao, washukiwa wengi walidai walipigwa na kujeruhiwa.
Washukiwa zaidi ya 20 hawangeweza kusimama hata kuingia ndani ya ukumbi wa korti walitambaa kama mtoto kwa vile miguu haikuwa na nguvu ya kutembea.
“Washukiwa wengi hapa wamepigwa wanauguza majeraha ya viungo. Wengine wamepigwa na kuteswa na hata hawawezi kuenda haja kubwa kutokana na uchungu na maumivu waliyo nayo,” mawakili 17 wakiongozwa na Levi Munyeri waliamba korti.
“Jinsi unavyowanaona washukiwa, wanauguza majeraha, wameteswa na kupigwa bila huruma na maafisa wa polisi,” wakili Levi Munyeri alimweleza hakimu.
Bw Munyeri pamoja na mawakili Suyianka Lempaaa, Wahome Thuku na Hosea Mwanwa waliomba mahakama iwaachiliwe washukiwa waende hospitali.
Mahakama iliombwa iwazuilie washukiwa wanaochunguzwa kwa kushiriki maandamano ambapo waliwajeruhi maafisa wa polisi, kuharibu mali na kuzuia polisi kutenda kazi yao.
Bw Munyeri aliomba mahakama iwaachilie washukiwa kwa vile Katiba Kifungu nambari 37 kinaruhusu wananchi kuandamana.
Katika uamuzi wake aliotoa saa tano unusu usiku Jumatano katika mahakama ya Milimani, Bi Nyamu alisema “upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuwanyima dhamana.”
Bi Nyamu aliwaachilia washukiwa wanne waliokamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabete.
Hakimu aliwapa dhamana ya Sh10,000 watoto 18 walio na umri uliochini ya miaka 18.
Washukiwa wengine waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000.
Katika dhamana hizi, hakimu alisema ni wazazi ama walezi wa watoto hao watakaozitia hati za kuwachilia kwenye vituo vya polisi.
Hakimu aliamuru washukiwa hao warudishwe vituo vya polisi vya Muthangari, Gigiri, Capitol Hill na Kilimani kuachiliwa.
Washukiwa hao walikamatwa na kufikishwa kortini kwa madai waliwapora wafanya biashara, kuharibu mali na kuzuilia polisi kutekeleza majukumu yao.
Pia walidaiwa walileta majeneza 14 ambayo waliweka vizuizi barabarani.
Kufikia sasa watu zaidi ya 30 waliuawa na polisi na wengine 361 kujeruhiwa na 627 kujeruhiwa.
Biashara ziliporwa na magari kadhaa ya polisi kuteketezwa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.