Habari za Kitaifa

Bukayo Saka wa Arsenal asaidia kuibeba Uingereza hadi nusu fainali Euro 2024

Na FATUMA BARIKI July 6th, 2024 1 min read

NYOTA wa Arsenal Bukayo Saka ameisaidia timu yake ya Taifa, Uingereza kufuzu kwa nusu fainali za kipute kinachoendelea cha Euro 2024.

Uingereza ambayo ilikuwa inamenyana na Uswisi iliyo na nyota Manuel Akanji, Xherdan Shaqiri na Granit Xhaka walionyesha mchezo vuguvugu kwa kipindi kirefu kwenye robo fainali hiyo ya tatu kwenye dimba hilo linaloendelea nchini Ujerumani.

Uswisi walikuwa na mchezo safi, huku pasi zao za kuonana zikiishia kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 75 wakati Dan Ndoye alipochonga krosi kali iliyoishia kwenye kisanduku cha Uingereza, na kumpata Breel Embolo, aliyesukumia kimnyani na mambo yakawa Uswisi moja, Uingereza sufuri.

Lilikuwa bao lililoweka hofu kambi ya kocha Gareth Southgate huku muda wa kawaida ukiyoyoma, na kudhihirisha kwamba huenda wakaaga dimba hilo huku Uswisi wakiingia kwenye nusu fainali yao ya kwanza kwenye dimba hilo.

Lakini katika dakika ya 80 wakati matumaini ya Uingereza yalikuwa yanaanza kufifia, mshambuliaji wa Arsenal Bukayo Saka alichenga wachezaji wa Uswisi na akiwa kwenye ncha ya kisanduku akaachilia mkwaju mrefu uliogonga mchuma na kujaa ndani ya wavu na kufanya mambo kuwa 1-1, jambo lililoinua pakubwa nyoyo za mashabiki wa timu hiyo ambayo ina historia ya kusuasua kwenye mashindano ya haiba kubwa.

Kufikia mwisho wa dakika zingine 30 za ziada, bado ilikuwa sare na hivyo ikamaanisha kwamba mchezo ungeamuliwa kupitia kwa mikwaju ya penalti.

Hapo napo wakali wao Cole Palmer (Chelsea), Jude Bellingham (Real Madrid), Saka (Arsenal), Ivan Toney (Brentford) na Alexander Arnold (Liverpool) wakafunga mikwaju yao yote huku mkwaju wa Akanji ukinyakwa na kipa Jordan Pickford, hivyo ikamaanisha Uingereza wamefuzu kwa nne bora kwa mabao 5-4 ya penalti.

Uingereza sasa itajua itakutana na nani kati ya Uholanzi na Uturuki ambao wanamenyana kuanzia saa nne usiku, Jumamosi, Julai 6, 2024.