Habari za Kitaifa

Hatutaki mazungumzo yenu, Gen Z waambia Ruto na Raila


VIJANA wamekataa wito wa Rais William Ruto wa kushirikisha wanasiasa katika mdahalo uliopangwa wa sekta mbalimbali unaolenga kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na Gen Z baada ya maandamano yao ya wiki tatu.

Matukio ya hivi punde yanajiri baada ya Rais na kiongozi wa Azimio Raila Odinga kutangaza Jumanne kuwa wameafikiana kuhusu mpangilio mpana wa kisiasa wa kutoa mustakabali wa kuondoa nchi kutoka kwa mzozo unaoikumba kwa sasa.

Hata hivyo, kushirikishwa kwa wanasiasa katika kongamano la siku sita la mazungumzo kumeibua mzozo mkubwa kutoka kwa makundi tofauti yanayowakilisha vijana ambao wameshutumu wanasiasa kwa kuteka mapambano yao.

Katika taarifa kali Jumanne, vijana hao walimshutumu Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa kujaribu kuteka harakati zao kwa kuunga mkono wanaowakandamiza.

Vijana hao walisema haitakuwa kama kawaida kwani wamejiandaa kwa mageuzi na hakuna kitakachowanyamazisha.

“Mpendwa Raila Odinga, uamuzi wako wa leo wa kusimama na wakandamizaji ulithibitisha chaguo letu la kutotaka uhusike na maandamano yetu tangu mwanzo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

“Hatutakuruhusu kuteka vuguvugu letu ili kukidhi uroho wako wa kisiasa. Hauzungumzi kwa ajili yetu na leo umeonyesha kuwa unasimama na wezi na wauaji. Hatutanyamazishwa. Hali sio kama uliyozoea,” taarifa hiyo iliongeza.

Gen Z walisema kwa wiki zilizopita, wamepigania haki zao, barabarani na mtandaoni, na wamelipa gharama hiyo huku makumi ya watu wakitekwa nyara, kuteswa na kuuawa.

“Hii haikuwa bure. Hatutajadiliana na wanaotutesa. Tunataka mabadiliko na tunayataka sasa.”

Rais Ruto alikuwa amesema kuwa kongamano hilo la siku sita, ambalo linatazamiwa kuandaliwa kati ya Julai 15 na 20, 2024, litapendekeza njia ya nchi kusonga mbele.

“Haya ni matokeo ya mashauriano ambayo tumepitia asubuhi ya leo na tunatarajia kuanza kongamano Jumatatu wiki ijayo,” kiongozi wa nchi alisema.

Bw Odinga aliongeza kuwa hatua ya kuafikiana kuhusu mazungumzo inafuatia mashauriano ya kina na Rais.

Rais William Ruto akiwa na wanasiasa wa upinzani akiwemo Kinara wa Azimio Raila Odinga, Jumanne. Picha|PCS

“Tumekubaliana kwamba mazungumzo ndio njia ya kutoka kwa shida ambayo inatukabili leo katika nchi yetu. Tumekubali kuwapa watu fursa ya kusikilizwa ili suluhu ya kudumu ipatikane. Tunataka yawe mazungumzo ya kusonga mbele ili tushughulikie masuala ya kimsingi ambayo yanaathiri jamii yetu leo,” alisema kiongozi huyo wa chama cha ODM.

Kiongozi wa Azimio alisema kuwa mazungumzo ndio njia pekee ya kusonga mbele ambayo serikali inaweza kutumia kuiondoa nchi kutoka kwa mzozo.

Alisema kuwa nchi iko tayari kusikiliza malalamishi ambayo Gen Z wamekuwa wakitoa katika siku za hivi karibuni.

“Tunatakiwa kuanza kwa kutambua na pili kuja na suluhu za matatizo haya. Tunafikiri kwamba kongamano hili litatusaidia kusonga mbele,” Bw Odinga alisema.

Bw Odinga pia alisema kuwa masuala ya ukosefu wa ajira, ufisadi, madeni, na usimamizi wa uchumi ni miongoni mwa masuala yatakayoangaziwa katika kongamano hilo.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alisema nchi iko katika njia panda na hakuna njia ambayo mapinduzi ya Gen Z yanaweza kupuuzwa.

“Wakenya wengi walitaka tufungue nafasi ya mazungumzo lakini hilo limefanywa na Gen Z. Tusipokuwa makini sote tutatupwa nje na Gen Z kwa vile wanasema tumezeeka,” akasema Bw Musyoka.

Kwa mujibu wa Rais, jopo hilo litaundwa na wajumbe 150 wanaowakilisha wadau mbalimbali, kati ya hao 50 watakuwa ni vijana.

Nafasi 100 zilizosalia zitawakilisha sekta nyingine zikiwemo mashirika ya kidini, Mashirika ya kijamii, vyama vya wataalamu, pamoja na vyama vya siasa.

Lakinii, taarifa nyingine kutoka kwa Gen Z na Millennials wasio na kiongozi walisema vijana hawaridhiki tena na mazungumzo au ahadi tu lakini wanataka hatua za haraka na thabiti.

Kundi hilo lilisema limetamaushwa na hali ya mambo nchini kwa sasa kwani malalamishi yao yamekabiliwa na kutojali.

“Tunawakilisha kizazi ambacho kinathamini matokeo. Msimamo wetu uko wazi: hatuna viongozi, hatuna chama na hatuna kabila. Utiifu wetu ni kwa mustakabali wa taifa hili, na tunadai haki yetu.”