Mnaosema nijiuzulu msubiri hadi 2027 tupambane debeni, Ruto ajibu shinikizo
RAIS William Ruto amewaonya baadhi ya viongozi wa kisiasa dhidi ya kuvuruga serikali yake kwa kuchochea maandamano akiwataka kusubiri hadi 2027 wapambane naye debeni.
Akiongea Jumatano, Julai 10, 2024 katika eneo bunge la Kajiado Magharibi, Kaunti ya Kajiado, Dkt Ruto alisema uchaguzi huo utakuwa ni kama mtihani kwa utendakazi wa serikali yake.
“Nataka waelewe kwamba 2027 tutafanyishwa mtihani na hawa wananchi na atakuja na yale ameyafanya. Kwa hivyo, tusisumbuane kabla ya hapo, tusubiri huu mtihani ili tuone ni nani atapita na nani wa kuanguka,” akasema.
“Taifa letu ni la kidemokrasia na wananchi, ambao ni werevu, wataamua wale viongozi watakaoenda nyumbani na wale wataopita katika uchaguzi. Mimi najipanga ili tukutane katika uchaguzi ujao, na hamna shida,” Dkt Ruto akaongeza akiwaonya viongozi hao, ambao hakuwataja, dhidi ya kutumia njia za mkato, za fujo, kuingia mamlakani.
Rais alisema hayo alipofungua rasmi kituo cha umeme cha Kimuka katika eneo bunge hilo la Kajiado Magharibi.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Dkt Ruto kujibu miito ya vijana wa Gen-Z na baadhi ya viongozi wa upinzani ya kumtaka ajiuzulu.
Baada ya vijana waandamanaji kuvamia majengo ya bunge Juni 25, 2024 baada ya kukerwa na hatua ya wabunge kupitisha Mswada wa Fedha wa 2024, Rais alitaja kitendo hicho kama uhaini.
Aidha, akijibu maswali kwenye mahojiano kati yake na wahariri wa runinga za NTV, Citizen na KTN, Dkt Ruto alidai kuwa fujo hizo zilipangwa na wanasiasa fulani aliosema wanachunguzwa.
Madai sawa na hayo yamewahi kutolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na mwenzake wa Ulinzi Aden Duale.
Jumatano, Rais Ruto aliwataka viongozi wa kisiasa, ambao hawakutaja majina, na Wakenya kwa ujumla, kudumisha amani na kukoma kujihusisha katika vitendo vya fujo.
“Kenya ni taifa linalozingatia utawala wa kidemokrasia na wale watakaoongozwa wanachaguliwa moja kwa moja na raia katika uchaguzi. Kwa hivyo, nawaomba viongozi wakome kuchochea fujo bali wasubiri uchaguzi 2027,” akasisitiza.
Hata hivyo, vijana wa Gen-Z wamekuwa akishikilia kuwa walifanya maandamano kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ungechangia kuongezwa kwa viwango vya ushuru na utawala mbaya wa Rais Ruto na kwamba hawakuchochewa na mtu yeyote.