Habari za Kitaifa

Kufuta mawaziri kwakosa kuridhisha Gen Z, waorodhesha matakwa mapya kwa Ruto

Na CECIL ODONGO July 12th, 2024 2 min read

KUVUNJA baraza la mawaziri bado hakujaridhisha Gen Z na itabidi Rais William Ruto atakeleze mabadiliko katika idara ya usalama.

Kulingana na Mchanganuzi wa Kisiasa Martin Andati, hatua aliyochukua Rais imekawia sana na kuna mengi ambayo bado hayawaridhishi vijana hao katika serikali.

“Vijana wanakamatwa na wanapotea katika njia tatanishi, makatibu katika wizara mbalimbali lazima awapunguze na awafukuze washauri wake ambao ni wengi. Haya ni kati ya mambo ambayo Rais lazima atimize, kwa hivyo safari bado,” anasema Bw Andati.

Mchanganuzi huyo anasema huenda ni mawaziri wanne au watatu pekee ndio watarejea katika baraza jipya la mawaziri japo vijana wengi lazima washirikishwe.

Mitandaoni, Gen Z walisema mkoko ndio kwanza ulikuwa ukialika maua na wanatarajia kuandaa maandamano makubwa mnamo Julai 16 kushinikiza serikali kutimiza matakwa yao yote.

Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri wake wote kufuatia shinikizo kutoka kwa vijana ambao wamekuwa wakiandamana kupinga utawala wake.

Aliwatimua mawaziri 21 na Mwanasheria Mkuu Justin Muturii huku akimsaza tu Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.

Naibu Rais Rigathi Gachagua pia amesalia serikalini kwa kuwa Katiba ya 2010 haimpi Rais mamlaka ya kumtimua naibu wake jinsi ilivyokuwa kwenye katiba ya zamani.

“Baada ya utathmini wa kina na kusikiza yale Wakenya wamekuwa wakisema, na kuchunguza utendakazi wa baraza langu la mawaziri, leo nimewafuta kazi mawaziri wote na Mwanasheria Mkuu,” akasema Rais Ruto.

“Afisi za Kinara wa Mawaziri ambaye ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Afisi ya Naibu Rais hazijaathirika kivyovyote vile,” akaongeza.

Mawaziri waliofukuzwa serikalini na sasa ni raia wa kawaida ni Profesa Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Susan Nakhumicha (Afya), Eliud Owalo (Teknolojia na Mawasiliani), Ababu Namwamba (Michezo), Florence Bore ( Leba), Salim Mvurya (Madini), Simon Chelugui (Ushirika na Mikopo) na Davis Chirchir wa Kawi.

Wengine ni Ezekiel Machogu (Elimu), Mithika Linturi (Kilimo), Penninah Malonzo (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Zacharia Njeru (Maji), Soipan Tuya (Misitu) na Kipchumba Murkomen.

Shoka la Rais pia halikuwasaza Rebecca Miano (Biashara), Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na Dkt Alfred Mutua ambaye alikuwa waziri wa Utalii.

Mwanasheria Mkuu Justin Muturi pia hakusazwa huku Rais akitangaza kuwa makatibu watakuwa usukani kabla ya kubuni baraza lake jipya la mawaziri.

“Kwa sasa, nitashauriana na watu kutoka sekta mbalimbali ili kuibuka na serikali pana ambayo itanisaidia kupambana na changamoto za nchi. Kati ya changamoto hizo ni mikakati ya kupunguza deni la kitaifa, kubuni nafasi za ajira, kupambana na ufisadi na kupunguza gharama ya serikali,” akaongeza Rais.

Vijana wamekuwa wakiandaa maandamano nchini kushinikiza serikali kukumbatia mageuzi na kati ya masharti waliyomwekea Rais ni kuwa avunje baraza lake la mawaziri.

Kilele cha maandamano hayo kilikuwa mnamo Juni 25 ambapo vijana walivamia Bunge kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024/25 ambao ulikuwa ukiungwa mkono na mrengo wa serikali.

Rais Ruto alionekana kunywea na kuondoa mswada huo uliokuwa na mapendekezo mengi ya kuongeza ushuru kwa raia, serikali ikilenga kuongeza mapato yake.

Katika wiki tatu ambapo maandamano hayo yamekuwa yakiendelea zaidi ya Wakenya 39 wameuawa kulingana na takwimu za Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (KNHCR).

Kile ambacho kiliwachochengea mawaziri wengi ni kiburi huku baadhi wakionekana kuwacheka Wakenya na kuwaonyesha utajiri wao.

Baadhi walikuwa wakitumia lugha ya kuwadhihaki raia ambao walikuwa wamelemewa na makali ya ugumu wa kiuchumi.

Bw Murkomen aliwakera Wakenya alipojinata kwa kuvaa saa ya Sh900,000 na mshipi ambao ulikuwa kati ya Sh40,000-Sh50,000, viatu vya kati ya Sh70,000-Sh80,000 na tai ya Sh20,000.

Bw Kindiki naye alipigwa fimbo na Wakenya baada ya kuwarejelea Gen Z waliokuwa wakiandamana kama wahalifu ambao wanahujumu usalama wa nchi.

Namwamba naye hakuhepa kero za Wakenya waliodai alikuwa akitumia wadhifa wake vibaya kwa kuandamana na watu wengi ambao hawafanyi lolote Kenya ilipokuwa ikishiriki mashindano mbalimbali nje ya nchi.