Kimataifa

Trump ajeruhiwa sikio baada ya kufyatuliwa risasi akiwa jukwaa la kampeni Amerika

Na LABAAN SHABAAN July 14th, 2024 1 min read

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump alijeruhiwa Jumamosi jioni alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara mjini Butler, Pennsylvania.

Katika kipindi hicho ambapo milio ya risasi ilisikika, damu ilionekana usoni mwa Trump na kwenye sikio lake upande wa kulia.

Haya yanajiri wakati kampeni za urais zinashika kasi nchini humo.

Trump, ambaye alikuwa rais wa 45 wa Amerika sasa ni mgombea mtarajiwa kwa tiketi ya chama cha Republican.

Huku hali ya wasiwasi na purukushani ikitanda baina ya milio ya risasi, Trump alionekana akishika sikio lake kabla ya kuinama na kuzingirwa na maafisa wa usalama.

Baadaye walinzi wake wakamwondoa jukwaani na kumpeleka katika gari lililokuwa karibu kisha msafara ukaondoka halahala.

Akiondoka jukwaani, Trump alikuwa akiinua mkono wake kuonyesha ishara ya ushindi.

Trump yuko salama

Idara inayosimamia ulinzi wa rais ilitoa taarifa ikisema Rais wa zamani Trump yuko salama.

Kadhalika, kikosi chake cha kampeni kilithibitisha kuwa yuko salama na alikuwa akipokea matibabu katika kituo cha afya.

Mfyatuaji Risasi Ameangushwa

Kulingana na maafisa wa usalama walionukuliwa na shirika la habari la Reuters, mshambuliaji huyo hatakuwa tishio tena.

Maafisa hao walisema: “Aliyefyatua risasi si tishio tena.”

Ikulu ya White House ilitangaza kuwa Rais Joe Biden alikuwa amepewa taarifa kuhusu tukio hilo.

“Vurugu za kisiasa hazikubaliki nchini Amerika,” Rais Biden alisema.

Trump kutangazwa mwaniaji urais

Tukio hili linajiri siku moja kabla ya kongamano kuu la chama cha Republican ambalo limeratibiwa kufanyika kuanzia Jumatatu mjini Milwauke, Wisconsin.

Katika mkutano huu, Trump anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa mgombea urais kabla ya uchaguzi wa Novemba mwaka huu.