Habari za Kitaifa

Ford Foundation yamjibu Ruto: Hatufadhili maandamano dhidi ya serikali yako


SHIRIKA la kutoa misaada lenye makao yake makuu nchini Amerika, Ford Foundation, limekanusha madai yaliyotolewa na Rais William Ruto kwamba lilifadhili maandamano ya kupinga serikali ya Kenya.

Katika taarifa rasmi, Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) lilifafanua kuwa halifadhili shughuli hizo na lina msimamo wa kutoegemea upande wowote katika juhudi zake zote za kutoa ruzuku.

“Hatufadhili wala hatujafadhili maandamano ya hivi majuzi dhidi ya mswada wa fedha na tuna sera isiyoegemea upande wowote kwa utoaji wetu wote wa ruzuku,” alisema Tolu Onafowokan, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa wakfu huo, akijibu Taifa Leo.

Rais Ruto, akiwa katika ziara ya kimaendeleo mjini Nakuru mnamo Jumatatu, aliitaka shirika hilo lisilo la kiserikali kwa kufadhili waandalizi wa maandamano dhidi ya serikali. Alionya wanaofadhili maandamano hayo kuzua vurugu nchini watakabiliwa na sheria.

“Tunaomba Wakfu wa Ford kueleza Wakenya jukumu lake katika maandamano ya hivi majuzi. Iwapo (Ford Foundation) hawapendezwi na demokrasia nchini Kenya, wanapaswa kuondoka. Tutawafichua wale wote ambao wana nia ya kurudisha nyuma demokrasia yetu iliyopatikana kwa bidii,” rais alisema akiwa Kuresoi.

Wakfu wa Ford ulikubali haki ya Wakenya kuandamana kwa amani lakini ulijitenga na aina yoyote ya vurugu.

“Ingawa tunatambua haki ya Wakenya kutetea kwa amani nchi yenye haki na usawa, tunakataa vitendo au matamshi yoyote ya chuki au kuchocheaa ghasia dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi au jamii. Kama tulivyosema wakati wa ziara ya serikali ya Kenya nchini Amerika mwezi Mei, tumejitolea kuendeleza urithi wa Wakfu wa Ford wa zaidi ya miaka 60 katika eneo hili ili Wakenya waweze kufungua fursa ambazo zinafaidi wote,” ilisema taarifa hiyo.

Shirika hilo pia lilisisitiza ahadi yake ya kihistoria na linaloendeleza kwa Kenya tangu 1963, ikiwa ni pamoja na msaada kwa watumishi wa umma, utaalam wa kiufundi, sekta ya elimu, na mipango mbalimbali ya mashirika ya kiraia.

“Tunadumisha dhamira ya kusaidia maendeleo ya Kenya na uongozi wa Kenya katika Afrika na kimataifa, ikidhihirishwa na usaidizi wetu kwa Mkutano wa kwanza wa Hali ya Hewa wa Afrika uliofanyika 2023, Nairobi na uongozi wa sasa wa Kenya kama mwenyekiti mwenza wa  Ushirikiano wa Uwazi wa Serikali,” Bi Onafowokan alisema.