Wezi wa mifugo wageuza Meru ‘ATM’ kwa kuiba mifugo kwa urahisi
MAJANGILI sasa wanarejelea Kaunti ya Meru kama ATM yao wakisema ni rahisi sana kuiba mifugo katika eneo hilo.
Haya yanajiri huku wizi wa mifugo ukiongezeka kwenye mpaka wa Meru-Isiolo.
Wakiwa na bunduki, majangili hao walivamia eneo la malisho la kaskazini lenye ukubwa wa kilomita 265 na kuiba ng’ombe na mbuzi.
Wiki iliyopita, licha ya usalama kuimarishwa, majangili hao waliiba ng’ombe, mbuzi na kondoo 819 katika uvamizi sita ambao ulizua mapigano yaliyodumu kwa saa kadhaa.
Ujambazi huo umeendelea kwa miaka mingi huku wafugaji wakipata hasara kubwa.
Mnamo 2019 wafugaji hao waliiomba serikali kuwalipa Sh374 milioni kama fidia ya mifugo iliyoibiwa.
Katika shambulio la hivi majuzi la mchana wiki iliyopita, majambazi hao waliwakabili polisi na askari katika mapigano yaliyodumu kwa saa 10 kabla ya kuwaokoa zaidi ya ng’ombe 150 huko Ngaathu, Igembe Kaskazini.
Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki aliahidi kutangaza mkoa wa Igembe kuwa eneo hatari na kusema serikali itaanzisha operesheni ya usalama ili kuleta amani katika eneo hilo.
Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Meru, Jacob Ouma, Jumatatu alisema polisi kufikia sasa wamepata ng’ombe na mbuzi 582 walioibwa wiki jana.
Uvamizi huo pia ulisababisha vifo vya wafugaji watatu na afisa mmoja wa polisi huku wengine kadhaa wakiuguza majeraha ya risasi.
“Uvamizi huo ulitokea kati ya Julai 6 na Julai 12 lakini tumefanikiwa kupata ng’ombe 556, Mbuzi 21 na kondoo 5. Tunawahakikishia wafugaji wetu kwamba timu za usalama sasa zimejitayarisha vilivyo kukabiliana na uvamizi huo,” Bw Ouma alisema.
“Walikuwa wakivamia maeneo tofauti kwa vipindi vifupi ili kuwachanganya polisi. Pia wanawazuilia maafisa wa usalama hadi giza liingie ili wasifuatwe na APC. Giza linapoingia, ni rahisi kwao kuona APC,” Bw Festus Gichunge, mfugaji alisema.
Baada ya kufanya uvamizi wao wa kwanza katika mwezi wa Julai 6, majambazi hao waliwashambulia wakazi tena Jumapili.
“Tumegundua kwamba majambazi hao wako kwenye kikundi na kila kikundi kina watu 20. Kuna kundi ambalo hushambulia huku wengine wakijificha kuwasaidia wenzao walioumia. Mapigano yakitokea, kundi lingine hukimbia na mifugo iliyoibwa,” Gichunge alisema.
Mwenyekiti wa wafugaji wa Ndumuru Genesio Gitonga, alisema majambazi hao pia wanatumia mbinu ya kutisha kama vile kuua wakazi ili kuleta hofu.