Habari Mseto

Mwangaza gizani tena madiwani wakilenga kumtimua mamlakani kwa mara ya nne

Na DAVID MUCHUI July 18th, 2024 2 min read

GAVANA wa Meru, Kawira Mwangaza, huenda akaondolewa mamlakani katika jaribio la mara ya nne, madiwani mara hii wakimlaumu kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya ofisi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hoja ya kumtimua, ambayo inakuja wiki tatu kabla ya maadhimisho ya miaka miwili ya Bi Mwangaza kama mkuu wa kaunti, inajumuisha malalamishi 11.

MCA mteule, Zipporah Kinya, jana aliwasilisha notisi ya hoja ya kuanza mchakato wa kumwondoa mkuu huyo wa kaunti ofisini.

Kuwasilishwa kwa mashtaka hayo kunajiri huku wakazi tisa wakimuomba Rais William Ruto asimamishe kaunti hiyo akisema kuwa serikali imeshindwa kutimiza kanuni za ugatuzi.

Bunge hilo kwa mara ya kwanza lilijaribu kumuondoa mamlakani Gavana Kawira Novemba 2022, takribani miezi minne baada ya kuingia madarakani kabla ya ombi hilo kusimamishwa na mahakama kwa kukosa ushiriki wa umma.

Hata hivyo, madiwani waliwasilisha hoja ya pili muda mfupi baadaye na kumshtaki gavana huyo kabla ya kuokolewa na Seneti mnamo Desemba 2022.

Miezi kumi baadaye mnamo Novemba mwaka jana, wawakilishi wa wadi waliwasilisha hoja nyingine ya kumuondoa ambayo pia ilikataliwa na Seneti.

Mnamo Jumatano, Bi Mwangaza aliarifiwa kuhusu madai hayo ambayo ni pamoja na kubatilisha uteuzi wa Katibu wa Bodi ya Utumishi wa Umma katika Kaunti Virginia Kagwiria kinyume cha sheria, kukosa kuwateua wenyeviti mbalimbali wa bodi zinazojitegemea na kukosa kutekeleza maazimio ya Bunge la Kaunti.

Mengine ni kumfukuza kazi mshauri wake wa kisheria kinyume cha sheria, kuwafuta kazi mawaziri kadhaa wa bodi kinyume cha sheria, na kuteua wakili wa kaunti bila kuchunguzwa na Bunge la Kaunti.

Gavana huyo wa Meru pia anadaiwa kuwalipa madaktari marupurupu ya Sh74 milioni na kuajiri wafanyakazi 111 wa kibinafsi na kusababisha malipo ya mishahara ya Sh500 milioni na kulipa takriban Sh103 milioni za mishahara kinyume cha sheria.

Lakini akizungumza na kituo kimoja cha redio nchini Jumatatu, Bi Mwangaza alisema bado anaunga mkono kusimamishwa kwa serikali ya kaunti na uchaguzi mpya kufanyika.