Habari Mseto

Vinara waliosalia Azimio waanza kuchora mustakabali wao bila Raila


VIONGOZI wa Azmio la Umoja-One Kenya Alhamisi, Julai 18, 2024, walikutana kujadili mustakabali wao baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuonyesha waziwazi kwamba chama chake kimeamua kufanya kazi na serikali.

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua alipakia picha mbili kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya X akiwa na wenzake kwenye mkahawa mmoja wakionekana kupanga mikakati.

Pamoja naye ni; kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa (DAP-Kenya), Charity Ngilu (Narc), Peter Munya (PNU) na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua, ambaye ni mshirika wa karibu zaidi wa Bw Musyoka pia ameketi kwenye meza mmoja na watano hao, katika mahala hapa panapoonekana kama mkahawa mmoja jijini Nairobi.

Bi Karua, ambaye mwa muda mrefu amekuwa akikwepa kuhudhuria mikutano ya Azimio, ameandamanisha picha hizo na kauli; “Definitely not boarding” (Bila shaka hatuabiri).

Kiongozi huyo wa Narc Kenya, ambaye alikuwa mgombeaji mwenza wa Odinga katika uchaguzi wa urais wa 2022, bila shaka anamaanisha kuwa katu hawatakubali matakwa ya Rais William kuhusu mazungumzo na kuundwa kwa serikali ya muungano wa kitaifa (GNU).

Vinara hao wamekutana siku saa chache baada ya wahuni walioaminika kuwa wafuasi wa  ODM kuvuruga hotuba ya Bw Musyoka baada ya mkutano wa kundi la wabunge wa Azimio katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (JOOF), Nairobi Jumatano jioni.

Vijana hao walizua vurugu punde tu kiongozi huyo wa Wiper alipoanza kusoma taarifa iliyosheheni msimamo wa Azimio kuhusu mazungumzo ya kujadili malalamishi ya vijana wa Gen- Z na pendekezo la Rais Ruto la kuunda serikali ya GNU itakayoshiriki upinzani na wadau wengine.

Kulingana na taarifa hiyo, Azimio ilikataa katakata kushirikishwa katika serikali ya muungano huku ukitoa masharti kadhaa kabla ya kushiriki katika mazungumzo hayo yaliyoitishwa na Rais Ruto.

Miongoni mwa masharti hayo ni kwamba vijana wote waliokamatwa wakati wa maandamano waachiliwe huru, polisi waliowaua baadhi ya wandamanaji wakamatwa, wafutwe kazi na kushtakiwa na serikali igharamie matibabu ya wale wote waliojeruhiwa katika maandamano hayo kote nchini.

Lakini Bw Odinga, ambaye aliongoza mkutano huo wa kundi la wabunge wa Azimio, hakuandamana na Bw Musyoka, na wenzake kwani ilidaiwa aliomba radhi kuhudhuria “jambo la dhararu”.

Isitoshe, viongozi wakuu wa ODM wakiwa manaibu wawili wa Odinga, Wycliffe Oparanya na Hassan Joho, kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi na mwenzake wa Seneti Stewart Madzayo, hawakuandamana na Bw Musyoka alipokuwa akisoma taarifa hiyo.

Hiyo ilikuwa ishara tosha, kwamba mrengo wa ODM katika Azimio, haukutaka kujihusisha na msimamo huo wa kukataa kujiunga na serikali ya Rais Ruto.