Maandamano yachacha Sudan, 800 wakamatwa

MASHIRIKA NA PETER MBURU

ZAIDI ya watu 800 wametiwa mbaroni katika maandamano ya pingamizi dhidi ya serikali nchini Sudan, waziri mmoja wa ngazi ya juu katika serikali ya taifa hilo amesema.

Waziri wa usalama wa ndani Ahmed Bilal Osman Jumatatu alieleza bunge la nchi hiyo kuwa tangu mwezi uliopita, watu 816 wamekamatwa na kuzuiliwa.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa serikali kueleza idadi ya watu ambao wamekamatwa tangu maandamano yalipoanza katika miji na vijijini na hata kufika katika jiji kuu la Khartoum.

Jumapili, wafanyakazi kadha wa chuo kikuu cha Khartoum walikamatwa kwa kujiunga na maandamano yaliyoanza Desemba 19 kuhusiana na hatua ya serikali kuongeza bei ya mikate.

Maandamano hayo ya halaiki yamekuwa yakihatarisha uongozi wa Rais Omar al-Bashir ambaye amekuwa mamlakani tangu 1989.

Tangu mwaka uliopita, Sudan imekuwa ikishuhudia matatizo ya kiuchumi kutokana na upungufu mkubwa wa pesa za kigeni, huku bei ya vyakula na dawa ikipanda maradufu na mfumko wa bei kugonga asilimia 70.

Japo Rais Al-Bashir ameahidi kushughulikia shida hiyo, waandamanaji wameshikilia msimamo wao wa pingamizi.

Serikali imetangaza kuwa angalau watu 19, wakiwemo walinda usalama wawili wameuawa katika machafuko wakati wa maandamano, japo mashirika ya kutetea haki kama Amnesty International yanasema watu 37 wameuawa.

Bw Osman alisema kuwa majumba 118 yaliharibiwa wakati wa maandamano, yakiwemo 18 ambayo yanamilikiwa na polisi, huku magari 194 yakichomwa, 15 kati yake yakiwa ya mashirika ya kimataifa.

“Maandamano yalianza kwa Amani, lakini wakora fulani waliokuwa na ajenda fiche wakatumia fursa hiyo kuiba,” akasema waziri huyo, japo akitaja hali katika taifa hilo kuwa ‘tulivu’ kwa sasa.

Asasi za serikali za Sudan zimekuwa zikivamia viongozi wa upinzani, wanaharakati na wanahabari kama mbinu ya kuzuia kusambaa kwa maandamano.

Mikutano mingi ya kupinga serikali imekuwa ikiongozwa na wataalam kama madaktari, walimu na wahandisi, japo polisi wamekuwa wakivuruga kwa kutupa gesi za kutoa machozi kutawanya waandamanaji.

Habari zinazohusiana na hii

Ni kubaya 2022!