Habari za Kitaifa

Ruto arudisha mawaziri sita wa zamani kati ya 11 alioteua

Na FATUMA BARIKI July 19th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto amerudisha mawaziri sita wa zamani kati ya 11 aliotaja kwenye Baraza lake jipya la Mawaziri.

Majina ya 11 hao bado yatawasilishwa Bungeni ili kupigwa msasa kabla ya kuajiriwa rasmi kupitia hafla katika Ikulu ya Nairobi.

Rais Ruto amemteua tena Kithure Kindiki kwa wadhifa ule ule aliokuwa akishikilia wa Usalama wa Ndani, Aden Duale amerejea kwenye Wizara ya Ulinzi, Soipan Tuya pia akarejea kwenye Wizara ya Mazingira huku Davis Chirchir aliyekuwa katika Wizara ya Kawi akipata ya Barabara, naye Alice Wahome aliyekuwa katika Wizara ya Ardhi akipewa Wizara ya Ujenzi. Rebecca Miano aliyekuwa Wizara ya Uwekezaji na Biashara amepewa jukumu la kuwa Mwanasheria Mkuu.

Kati ya wapya watano alioteua ni Debra Barasa (Afya), Julius Migosi (Elimu), Andrew Muihia (Kilimo), Eric Muriithi (Maji) na Margaret Nyambura (Teknolojia).

Dkt Ruto alisema kwamba hii ni awamu ya kwanza ya uteuzi, ikimaanisha kwamba uteuzi wa wengine 11 utafanywa baadaye.

Haijafahamika bayana iwapo sura kamili ya “serikali jumuishi” aliyosema kwa msisitizo itadhihirika kwenye uteuzi ujao, haswa kukiwa na tetesi kwamba upande wa upinzani haswa mrengo unaoongozwa na Raila Odinga utajiunga na serikali.