Habari Mseto

Kawira aelekea kunusurika madiwani zaidi wakikunja mkia

Na DAVID MUCHUI July 22nd, 2024 2 min read

HOJA ya kumtimua Gavana wa Meru Kawira Mwangaza inaelekea kuporomoka baada ya madiwani 10 kujiondoa na kusema hawaiungi mkono.

Kujiondoa kwa madiwani hao ni nafuu kwa Bi Mwangaza ambaye sasa anaungwa mkono na madiwani 23, huku akihitaji mwakilishi mmoja tu zaidi ili aangushe hoja hiyo hata kabla haijawasilishwa.

Bunge la Kaunti ya Meru lina madiwani 69 ambapo 13 ni wandani wa Bi Mwangaza. Wiki jana, madiwani 54 walikuwa wameidhinisha mswada huo.

Kumng’atua Bi Mwangaza mamlakani, lazima hoja hiyo ipigiwe kura na madiwani 46, idadi ambayo ni theluthi mbili jinsi ambavyo inahitajika kisheria.

Hapo Jumapili, madiwani waliojiondoa walisema hoja hiyo imekuja wakati usiofaa ikizingatiwa kuwa kumekuwa na mazungumzo ya kupatanisha gavana huyo na wakosoaji wake.

Pia walisema bunge hilo linastahili kuipa kipaumbele kupitishwa kwa bajeti ya 2024/25. Bunge la kaunti la Meru bado halijapitisha bajeti ya 2024/25 kutokana na tofauti kuhusu mgao ambao unastahili kuendea kila wadi.

Hatua hiyo inakuja baada ya Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala kuamuru madiwani wake waindoe hoja hiyo.

Aidha kamati ya watu 25 wakiwemo wazee wa Njuri Ncheke na viongozi wa dini, iliyoundwa kumpatanisha Bi Mwangaza na wakosoaji wake, bado haijawasilisha ripoti yake kwa Rais William Ruto.

Kamati hiyo ililenga kutatua mzozo wa kisiasa ambao umekwepo katika Kaunti ya Meru.

Madiwani ambao walijiondoa ni Kithinji Ethaiba (Nkomo), Domiano Muchui (Igoji Mashariki), Jennifer Murogocho (Kiirua/Naari), Sarah Gakii (mteule), Caleb Mutethia (Municipality), Jacob Mwirigi (Kibirichia), Martin Kimathi (Timau), Harun Thuranira (Abogeta Mashariki), Patrick Mwirigi (Ntunene), na Felix Kithinji (Ruiri/Rwarera).

“Ni mtazamo wetu kuwa mswada wa kumwondoa mamlakani Gavana Kawira Mwangaza hufai na haujafikiriwa vyema. Bado hatujapata ripoti ya kamati ya upatanishi ambayo ilianzishwa mnamo Machi na pia hatujapitisha bajeti,” akasema Diwani wa Kibirichia Jacob Mwirigi.

“Vilevile  bado hatujapitisha bajeti na hili ni suala ambalo tunastahili kulipa kipaumbele. Tunaendelea kuongea na gavana ili kila mradi utengewe Sh33 milioni kwa miradi mbalimbali,” akaongeza.

Kamati hiyo ililenga kutatua mzozo wa kisiasa ambao umekwepo katika Kaunti ya Meru kwa muda mrefu tangu uchaguzi mkuu wa 2022.

Diwani wa Nkomo Kithinji Ethaiba alisema ni mapema sana kumtimua gavana kabla ya ripoti ya maridhiano kuwasilishiwa rais na kuwekwa wazi kwa umma.

“Kama kiongozi na mzee wa Njuri Ncheke, siwezi kuvuruga juhudi za upatanisho ambazo zinaendelezwa na Rais kupitia kamati iliyobuniwa. Tusubiri ripoti hiyo iwekwe wazi mwanzo,” akasema Bw Ethaiba.

Naye Katibu Mkuu wa Njuri Ncheke Josephat Murangiri alisema ripoti ya upatinisho ipo tayari na wanasubiri kuiwasilisha tu kwa Rais Ruto.

Bi Murogocho naye aliwataka wenzake wakome kufanya maamuzi ya haraka na kufikiria kila mara kumwondoa gavana na badala yake wajihusishe na mambo yanayowahusu raia.