Habari za Kitaifa

Kibarua cha Mbadi kutakasa Kenya Kwanza dhidi ya madeni na uchumi mbaya

Na SAMWEL OWINO July 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIBARUA kigumu kinamsubiri waziri mteule wa Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi John Mbadi ikiwa ataidhinishwa na bunge.

Bw Mbadi, mbunge mteule na mwenyekiti wa sasa wa Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Uhasibu wa Umma (PAC), atachukua nafasi iliyoshikiliwa na Prof Njuguna Ndung’u.

Akiidhinishwa, atachukua usukani wa wizara wakati ambapo serikali iko chini ya shinikizo la kupunguza ufujaji na pia kukabiliwa na maandamano kutoka kwa vijana wanaotaka uwajibikaji na matumizi ya wazi ya kifedha.

Kuna pego la Sh346 bilioni katika bajeti lililotokana na kukataliwa kwa Mswada wa Fedha, 2024 ambalo pia linangoja Bw Mbadi ikiwa ataidhinishwa kwani atalazimika kusawazisha matumizi kwa uangalifu kwa mwaka mmoja ujao.

Bw Mbadi atakuwa na jukumu la kubana pesa katika mwaka huu wa kifedha kwani atahakikisha kuwa hakuna ubadhirifu serikalini ambao ni mojawapo ya sababu za vijana kuandamana.

Pia anatarajiwa kusimamia deni la nchi na kupunguza gharama ya maisha.